Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtaka rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kutumbua majipu katika maeneo ambayo inatakiwa kufanya hivyo.
Mbali na ombi hilo, amesema atamuuzia wanyama kwa bei ya Serikali ili watengeneze eneo la kuhifadhia wanyama Zanzibar litakalotumika kuongeza mapato ya Serikali.
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 14, 2021 wakati akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika wilayani Chato Mkoa wa Geita baada ya kutembelewa na Dk Mwinyi na makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Viongozi hao wa Zanzibar wapo wilayani humo kwa ziara ya siku mbili.
“Mmeanza vizuri sana, sana, sana msiogope kutumbua majipu, wanaowakwamisha kwa ajili ya maendeleo ya watu fanya, na nikuombe Maalim Seif msaidie sana rais kuhakikisha masuala ya mali za umma, wanyonge zinasimamiwa kikamilifu.”
“Nina uhakika kwa mwendo huu mlioanza nao Zanzibar itakuwa Dubai nyingine kwa sababu mahali ambapo panahubiriwa amani na upendo, wawekezaji watakuja, sehemu ambapo hakuna rushwa wawekezaji watakuja,” amesema Magufuli.
Kiongozi huyo ameahidi kuwauzia baadhi ya wanyama kwa bei ya Serikali ili waweze kuanzisha Zoo kisiwani Zanzibar kwa sababu sheria zinaruhusu.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu ombi la Dk Mwinyi, “aliniomba kuwa na yeye awe na Zoo au ranchi wafuge wanyama kama swala, pundamilia. Nimewaambia hakuna tatizo tutawauzia kwa bei ya Serikali wafuge nao huko ila wasimalize wanyama wa huku.”
“Hata watalii wanapokuja waache hela kule kwa sababu pesa zinazopatikana Zanzibar zinakuwa pia ni za huku.”