Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio ya kodi na tozo zote zilizopo katika zao la mkonge kwa lengo la kubaini ni zipi zenye manufaa kwa wadau na Taifa na kuainisha zisizokuwa na tija ili zifanyiwe mchakato wa kuondolewa.
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati wa kikao chake na wadau wa mkonge mkoani Tanga, ambapo alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kufuatilia mwenendo wa mazao yote ya biashara nakuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania ishirikiane kikamilifu na kituo Kituo cha Utafiti wa Kilimo kuendelea kuboresha zao hilo.
Waziri Mkuu amesema serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao la mkonge linarudi katika nafasi yake, hivyo ameiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kuratibu maendeleo yake kuanzia hatua za utayarishaji mashamba hadi mwenendo wa masoko.
“Mkonge unafaida nyingi lakini sisi tumejikita katika utengenezaji wa nyuzi tu, tutumie wataalamu wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwa ajili ya kutumia fursa nyingine zinazopatikana katika zao hili kwa kutengeneza sukari, mbolea na vinywaji.” amesema Majaliwa
Aidha Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote zinazolima mkonge nchini pamoja na uongozi wa Bodi ya Mkonge kuanzisha kanzi data kwa ajili ya kuwa na takwimu za wakulima wadogo, wakati na wakubwa pamoja na ukubwa wa mashamba yao na itawasaidia kuwafikia wakulima kwa urahisi pale wanapotaka kutoa elimu kuhusu namna bora ya kulima zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba, matumizi ya pembejeo pamoja na upatikanaji wa masoko.