Makada 50 CCM wasimamishwa uongozi, wadaiwa kusababisha kura za urais kupungua


Geita. Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Geita nchini Tanzania imewasimamisha viongozi zaidi ya 50 wa chama hicho kwa madai ya usaliti katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2020 na kusababisha idadi ya kura za urais katika wilaya hiyo kupungua.


Waliosimamishwa ni viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia vijiji, mitaa, kata na wilaya.


Katika uchaguzi mkuu huo mgombea wa CCM, Rais John Magufuli alipata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa.


Kwa ushindi huo Magufuli alifanikiwa kutetea kiti hicho kwa muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, baada ya kuwashinda washindani wake 14 waliokuwa wakiwania kiti hicho.


Imeelezwa kuwa kupungua kwa idadi ya kura za urais wilayani humo kulisababisha chama kupata nafasi mbili za ubunge wa viti maalum tofauti na mikoa mingine waliopata wabunge watatu kutokana na wingi wa kura.


Katibu wa itikadi, siasa na uenezi wa chama hicho wilayani humo, Jonathan Masele ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 15, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wa halmashauri kuu ya chama.


Masele amesema katika uchaguzi huo walitegemea kupata wapiga kura zaidi ya 100,000 lakini wapiga kura waliojitokeza ni 56,000 tu katika wilaya yote yenye majimbo matatu na kudai baadhi ya wapiga kura hawakujitokeza kutokana na ushawishi wa wasaliti wa chama.


Amesema halmashauri kuu ya chama hicho imezitaka kamati za maadili ngazi ya wilaya, kata na vijiji kuwaita wote waliosababisha kutokea upungufu wa kura ili wahojiwe na hatua nyingine za kinidhamu ziweze kuchukuliwa.


“Watu hawakujitokeza kupiga kura licha ya kuwa ni haki yao ya msingi kumchagua kiongozi wanayemtaka..., kukaa ndani na kufikiri unayempenda ameshinda ndio imesababisha kura za wabunge wa viti maalum kuwa chache na hivyo tukapata wabunge wawili tu,” amesema Masele.


Masele amesema jimbo la Geita kura za jumla ilikuwa asilimia 24, Geita mjini asilimia 40 na Busanda asilimia 36.


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita,  Muhoja Mapande amesema licha ya chama kushinda kata na majimbo yote bado kura zilizopigwa zilikuwa chache na hiyo imetokana na wasaliti ambao hawakuridhika na uteuzi wa wagombea.


“Lazima tushughulike nao tutawaita kwenye vikao vya kikanuni tuwahoji na kuwachukulia hatua kwa kanuni ya adhabu kulingana na kosa alilotenda,” amesema Mapande.


Amesema chama kina adhabu mbalimbali  mwanachama anapobainika kusaliti ikiwemo kupewa onyo la mdomo ama maandishi, karipio, kuvuliwa uongozi au uanachama  na kwamba yote hulingana na kosa alilotenda.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad