Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.
Serikali imeyaonya makampuni ya simu ambayo watumishi wao wamekuwa sio waaminifu na wamekuwa wakivujisha siri za wateja wao kwa watu wengine huku ikitaka wananchi wenye malalamiko kama hayo kuyawasilisha Wizarani ili Makampuni hayo yachukuliwe sheria.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile wakati wa hafla ya kutiliana saini mikataba kati ya Makampuni ya simu na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ili kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini.
Waziri Ndugulile amesema kuna makampuni ya simu ambayo watumishi wao si waaminifu na wamekuwa wakivujisha siri za wataje kwa marafiki zao au kwa kuhongwa fedha.
"Kumekuwa na tabia kwenye haya makampuni watumishi wanavujisha siri za mawasiliano za wateja mtu kagombana na mpenzi wake anakuja kwenu mnamkopia mawasiliano yake yote hilo halikubariki" amesema Dkt Ndugulile.
Ameyataka Makampuni hayo kukomesha tabia hiyo na kuyataka yakasome vizuri mikataba yao waliyoingia na Serikali katika kutoa huduma hizo, amewataka wateja wote wenye malalamiko kama hayo kuyafikisha katika ofisi yake ili Makampuni hayo yachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha amezitaka Kampuni hizo kuanza kuangalia namna ya kuboresha huduma zao kwa kuondoa huduma ya interneti ya kasi ya 2G na ili kama nchi tuanzie kasi ya 3G na kuendelea mbele kama nchi nyingine pia akihimiza kupunguza gharama za bando kwa wateja wao.
Amebainisha kuwa ulimwengu tunaouendea utakuwa ni wa kimtandao zaidi na kuyataka makampuni hayo kuendelea kuboresha zaidi huduma zao ili tufikie malengo hayo mapema zaidi uchumi wetu uendelee kuimarika zaidi.
Amesema sekta hiyo inakuwa kwa kasi sana hapa nchini ambapo hadi sasa kuna laini milioni 50 zimesajiliwa kwa Mawasiliano na laini takribani milioni 24 zinatumia huduma ya interneti kote hapa nchini.
Ameyataka Makampuni kuheshimu mikataba hiyo waliyoisaini na haitasita kuwachukulia hatua watakaokiuka mikataba yao, na amewataka ambao hawajakamilisha mikataba ya awali kuimaliza haraka iwezekanavyo na hataki kuona miradi ambayo haikamiliki.
Ameongeza kuwa " Kama makampuni muanze kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia rahisi na sio kuwa na minara utitili na hii bei ya milioni mia tatu(300,000,000) kwa mnara mmoja ni kubwa Sana" amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF Justina Mashiba amesema mikataba hiyo ni awamu ya tano tangu kuanza kusainiwa na mikataba hiyo ni miezi 9 utavifikia vijiji 173 na kata 61 na ukikamilika utawafikia wananchi laki saba (700,000) katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema tangu kuanza kwa mfuko huo wamezifikia kata 1055 na vijiji 3025 katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kutambua kuwa watu wengi wanaishi vijiji nao wapate huduma kama watu wengine.
Amesema katika awamu hii wamelenga kuvifikia vijiji vingi zaidi ambapo Serikali imetoa bilioni 6 katika kufikisha mawasiliano katika maeneo mengi ya nchi, na kwa upande wa mipakani wameanza kwa baadhi ya mipaka kama Kigoma na Rombo na taratibu za kubaini maeneo mengine ya mipakani yanayohitaji huduma unaendelea.
Akiongea kwa niaba ya Makampuni mengine meneja ufundi kutoka Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Endrew Pembe amesema watahakikisha wanaheshimu mikataba hiyo na kufikisha huduma ya Mawasiliano katika maeneo yote waliyopangiwa kufikisha huduma.
Aidha amebainisha kuwa kama Makampuni ya simu wamekuwa wakifanya kila jitihada kuhakikisha wanatokomeza matapeli ambao wamekuwa wakisumbua wateja wao.
Serikali imeingia makubaliano na Makampuni matatu ya mawasiliano kwa ajili ya kufikisha mawasiliano katika maeneo ya pembezoni Makampuni hayo ni Tigo, Vodacom na Airtel.