Makato mikopo ya elimu ya juu sasa kaa la moto

 



Dar es Salaam. Wakati Chama cha ACT Wazalendo kikieleza kusudio la kwenda kupinga mahakamani mabadiliko ya Sheria Bodi ya Mikopo ya 2016, Wizara ya Elimu imeitaka Bodi hiyo kutoa ufafanuzi wa malalamiko yanayotolewa na wadaiwa.


Kwa upande wake Bodi hiyo (HESLB) imesema inatekeleza sheria jinsi ilivyo kwa kuwa ndiyo imepitishwa na Bunge na kwamba viwango vya makato vinavyolalamikiwa viliwekwa kwa kuwashirikisha wadau, vikiwemo vyama vya wafanyakazi.


Hata hivyo, HESLB haikutaja vyama vilivyoshiriki mchakato huo, ingawa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limekana kushirikishwa katika mchakato wa makato hayo.


Miongoni mwa malalamiko yanayotolewa na wadaiwa ni ongezeko la makato ya mkopo huo kutoka asilimia 8 hadi asilimia 15 kwa mwezi kutoka katika mshahara ghafi wa mdaiwa/mnufaika.


Mengine ni tozo ya kutunza thamani ya mkopo ya asilimia 6 (Value retention fee -VRF), tozo ya asilimia moja ya shughuli za kiutalawa (Loan Administration Fee) na adhabu ya asilimia 10 ya deni linalodaiwa kwa anayechelewa kulipa deni baada ya miaka 2 tangu kuhitimu chuo.


Kutokana na malalamiko hayo, ACT Wazalendo imesema imeiandikia barua Wizara ya Elimu na HESLB kueleza kusudio la kwenda kupinga mahakamani mabadiliko ya sheria hiyo.


 “Mnamo Januari 20, 2021 Katibu wa Ngome ya vijana ACT Wazalendo, Mwanaisha Mndeme aliandika barua kwenda Wizara ya Elimu na kuinakili kwa Ofisi ya Rais-Ikulu (kupitia Katibu mkuu kiongozi), Ofisi ya Waziri mkuu na HESLB,” imesema sehemu ya taarifa ya ACT.


Lakini akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Dk Akwilapo alisema hajapata barua hiyo.


“Kama ni suala hilo limeshatolewa ufafanuzi bungeni na hata Bodi (HESLB) imeshatoa ufafanuzi, watafute wakupe ufafanuzi,” alisema Dk Akwilapo.


Alipoulizwa kuhusu maelezo ya HESLB kuwa wanatekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge, Dk Akwilapo alisisitiza; “Hiyo sheria ilianzia hukohuko bodi, watafute wakupe ufafanuzi, hata mimi ninao.”


Taarifa iliyotolewa na Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo imesema “Viwango au makato haya yanafanya vijana kutopiga hatua yeyote. Pia ni kinyume na katiba yetu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 23(1) inayohitaji mtu kupata ujira kulingana na kazi yake,” imesema taarifa hiyo.


Mbali na ukubwa wa makato hayo, taarifa hiyo imesema baadhi ya waombaji waliingia mkataba na HESLB wa kukatwa asilimia 8 lakini baada ya mabadiliko ya sheria hiyo, sasa wanakatwa asilimia 15.


“Kwanini Serikali ibadili sheria inayovunja mkataba/makubaliano bila taarifa, maoni au mashauriano na wadaiwa au wanufaika?.


Mbali na ACT Wazalendo, Samuel Ngulinzira, mmoja wa wadaiwa aliyezungumza na Mwananchi kwa simu jana amesema aliingia mkataba na HESLB kukatwa asilimia 8, lakini kwa sasa anakatwa asilimia 15.


“Nilianza chuo mwaka 2013 na mkataba wangu ulisema nitakatwa asilimia 8, lakini baada ya kunaliza shule mwaka 2016, sheria imebadilika sasa nakatwa asilimia 15,” alisema.


“Tumeshalalamika kwa bodi, tumelalamikia makato ya asilimia 6, asilimia 1 na asilimia 10 yaliyoongezwa, lakini bodi inasema inatekeleza tu sheria.


“Tumepanga kwenda kulalamika bungeni,” aliongeza.


Kuhusu tozo ya asilimia 6 ya kutunza thamani ya mkopo (VRF), ACT imesema haina uhalisia.


“Hii si sawa sababu kushuka thamani kwa fedha yetu kwa mwaka haiwezi kuwa kwa asilimia sita, hiki ni kiwango kikubwa sana. Pia kuna usiri na kutoeleweka kwa mchanganuo wa namna ya kuipata hiyo asilimia 6,” imesema.


Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha HESLB, Omega Ngole aliwataka wanaolalamikia wasome vizuri mikataba yao.


“Awali Sheria ilikuwa inaipa Serikali mamlaka ya kupanga kiwango cha makato na kubadilisha wakati wowote. Mabadiliko ya sheria ya mwaka 2016 yamekuja na mambo mengi, kwanza yameweka moja kwa moja kiwango cha asilimia 15 hivyo Serikali haiwezi kubadilisha mpaka irudi bungeni,” alisema Ngole.


Pia alisema mabadiliko hayo yalisogeza muda wa kuanza kulipa (grace period) kutoka miezi 12 hadi 24. “Kama kuna mtu au taasisi ina maoni, yawasilishwe kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB au Wizarani na tutafanyia kazi,” alisema Ngole.

Majibu wa Tucta


“Vyama vya wafanyakazi havijawahi kushirikishwa kwenye mabadiliko hayo. Walioingia mkataba walikuwa wanafunzi, sasa vyama vya wafanyakazi vinaingiaje hapo?” alihoji Tumaini Nyamhokya, rais wa Tucta huku akidai kuulizwa na swali hilo na wengi.


“Ni kweli hata sisi hilo suala linatuuma, lakini msiibebeshe Tucta mzigo. Tumekuwa tukilisemea na tumewashauri watu wenye uwezo wasijiingize kwenye mikopo hiyo kwa kuwa siyo msaada tena,” aliongeza.


Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad