Mbunge mmoja wa chama cha Trump aahidi kutembea na bunduki wazi mitaani. Mbunge mpya mwanamke aahidi kutembea na bunduki wakati wa muhula wake huko Washington DC.
Katika video iliyotolewa Jumapili, mbunge wa Republican Lauren Boebert anaonekana akiweka bunduki yake ya mkononi risasi kabla ya kuanza kutembea nayo mjini.
“Nitabeba bunduki yangu nikiwa Washington DC na bungeni pia,” amesema katika video ambayo imetazamwa na watu zaidi ya mara milioni mbili.
Lakini mkuu wa polisi amesema anapanga kuzungumza na Bi. Boebert kuhusu sheria kali za kubeba bunduki.
Bi. Boeber ni mmiliki wa mgahawa unaojulikana kama ‘Shooters Grill mjini Rifle Colorado, ambako watu huamasishwa kubeba silaha zao wazi kwasababu kisheria huko, inaruhusiwa.
Suala la haki ya kumiliki bunduki ilikuwa sehemu ya msingi wakati wa kampeni yake katika uchaguzi uliofanyika Novemba.
“Hata kama sasa hivi nafanyakazi katika moja ya miji huru Marekani, siwezi kutupilia mbali haki yangu,” Bi. Boebert amesema katika video iliyowekwa kweye mtandao wa Twitter Jumapili.
“Kama mwanamke mwenye urefu wa futi tano, na uzito wa kilogramu 45, nina chagua kujilinda mweyewe kwasababu mimi ndio mlinzi mzuri kwangu binafsi.”
Hata hivyo polisi wamejibu kwa haraka huku mkuu wa polisi Washington DC Robert Contee III akiwaambia wanahabari: “Mbunge atakabiliwa na adhabu ile ile kama mtu mwingine yeyote anayepatikana akiwa amebeba silaha katika mji wa DC.”
Wakati katiba inaruhusu haki ya watu kumiliki na kuweka silaha, sheria zilizopo zinatofautiana kutoka mji mmoja hadi mwingine.
Wabunge wanaruhusiwa kumiliki bunduki katika ofisi zao na kusafiri nazo mjini Washindton DC mradi zisiwe na risasi.
Hata hivyo, kibali kinahitajika kwa mtu kubeba bunduki katika mitaa ya mji huo pamoja na kubeba silaha kutoka majimbo mengine lazima kwanza iwe imesajiliwa na mamlaka ya eneo.
Mwezi uliopita, kundi la maseneta wa Democrat walipendekeza sheria mpya kuimarisha sheria zilizopo za umiliki wa bunduki kwa wabunge.