Mbinu mpya zanasa vigogo wa dawa za kulevya



Dar es Salaam. Kubadili mbinu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kumezaa matunda na kufanikiwa kuunasa mtandao na mapapa wa biashara hiyo nchini pamoja na kukamata kiasi kikubwa cha heroini na cocaine kwa mwaka 2019.


Kabla ya mwaka huo, wengi waliokuwa wakikamatwa walikuwa ni wasambazaji wa mwisho na watumiaji ambao walikuwa wakinaswa na kiasi kidogo cha dawa, tofauti na ilivyo sasa ambapo nguvu zimeelekezwa kuwanasa vigogo, yaani wafanyabiashara wakubwa wanaohusika na mtandao wa uingizaji wa dawa hizo nchini.


Taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2019, inabaianisha kuwa awali wafanyabiashara hao walikuwa wakitumia viwanja vya ndege na mipaka rasmi kupititisha dawa hizo kutokana na mtandao iuiokuwepo kuhusisha pia baadhi ya watumishi wasiokuwa na uaminifu.


Hata hivyo, kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi na udhibiti katika maeneo hayo, kwa sasa wanatumia njia za panya ambazo pia zimegunduliwa na vyombo husika hadi kuwezesha kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha dawa hizo.


Taarifa hiyo inaonyesha jumla ya kilo 55.35 za heroini na kilo 10.34 za cocaine zikiwahusisha watuhumiwa 349, ikiwa ni idadi ndogo ya watuhumiwa ikilinganishwa na waliokamatwa mwaka uliotangulia.


Mwaka 2018 zilikamatwa kilo 16.94 za heroini na kilo 7.67 za cocaine zikihusisha jumla ya watuhumiwa 611. Mwaka uliovunja rekodi ni 2017 zilipokamatwa kilo 185.56 za heroini na kilo 4. 14 za cocaine.



Kulingana na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) ongezeko hilo la dawa zilizokamtwa limetokana na nguvu kuelekezwa kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo ambao hukutwa wakiwa na mzigo mkubwa.


Kamishna msaidizi wa Kinga na Tiba wa DCEA, Dk Cassian Nyandindi amezitaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni kuibaini mitandao ya wafanyabiashara hao na kuwakamata wakiwa na mzigo.


“Unapodeal (unapopambana) na dawa za kulevya hutakiwi kupiga kelele, mkakati wetu ni kwamba hata kama unafanya biashara hii hatutakuja kwako kukukamata hadi tuhakikishe mzigo unao na tukija tutakukuta nao. Operesheni zetu ni za kiitelejensia, si kukurupuka na ndio maana tunaowakamata kwa sasa ni wale `magiants’ (mapapa).


“Tanzania pia imeweza kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda ambapo tunapata taarifa za usafirishwaji wa dawa za kulevya na kuzifuatilia hadi kuwakamata wahusika, hasa wanaotumia njia za kwenye maji,” alisema Dk Nyandindi.


Aliitaja sababu nyingine ni utashi wa kisiasa wa Serikali iliyopo madarakani kwa kuweka nguvu kubwa katika vita dhidi ya dawa hizo na kuwezesha mamlaka hiyo kufanya operesheni zake kwa ufanisi.


Alichokisema kamishna huyo kinaendana na kilichoelezwa kwenye ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) iliyotolewa mwaka 2020 ambayo imeitaja Tanzania kufanikiwa kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90.


Ripoti hiyo imekwenda mbele na kueleza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa `Covid-19’ kwa mwaka 2020 katika mataifa mbalimbali ulichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza usafirishaji wa dawa hizo na kusababisha kuadimika mitaani kwa watu wa kawaida.


Dk Nyandindi alieleza kuwa katika operesheni zilizofanyika mwaka 2019 jumla ya watuhumiwa 349 walikamatwa kati yao 318 wakiwa wa heroini na 31 wa cocaine.


Sanjari na dawa hizo za viwandani, dawa za kulevya za mashambani ya aina ya bangi na mirungi nazo zimeendelea kusumbua na kuangamiza watu wengi.


Kulingana na taarifa hiyo ya hali ya dawa za kulevya mwaka 2019, tani 21.16 za bangi zilikamatwa ikiwa ni upungufu wa tani mbili ikilinganishwa na kiwango kilichokamatwa mwaka 2018 ambayo ni tani 23.61.


Kiwango hicho kiliwahusisha watuhumiwa 8,865 na mashamba ya bangi 31 yenye ukubwa wa ekari 22 yakiwa na jumla ya miche ya bangi 1,997 yaliteketezwa.


Upande wa mirungi tani 9.07 zilikamatwa sambamba na watuhumiwa 1,170 waliojihusisha na biashara hiyo, ambayo ni idadi ndogo ikilinganishwa na idadi ya watuhumiwa katika miaka mitano iliyopita.




Changamoto katika mapambano


Pamoja na mafanikio ambayo mamlaka hiyo imepata katika vita dhidi ya dawa za kulevya bado kuna changamoto ambazo zinasababisha dawa hizo kuendelea kuwepo.


Mojawapo ya changamoto hizo ni ukubwa wa mipaka ambapo Dk Nyandindi anaeleza kuwa bandari bubu zipo nyingi na zimekuwa zikitumika kupitisha dawa hizo.


Nyingine ni kubadilika kwa njia za usafirishaji ambapo kila kukicha wafanyabiashara wanabuni mbinu mpya, hata hivyo hubainika na ndiyo maana kiasi kikubwa cha dawa kimeendelea kukamatwa.


“Pia kuna shida ya utofauti wa sheria, mfano hapa kwetu ukikamatwa na dawa za kulevya unafungwa, nchi nyingine mfano Burundi ukikamatwa unalipa faini unaachiwa, hivyo mtu anaweza kuingizia Burundi hata akikamatwa atalipa faini kisha atatafuta njia ya panya ya kuziingiza hapa nchini,” alisema Dk Nyandindi.




Kesi zilizopo mahakamani


Kulingana na taarifa ya mwaka 2019 zaidi ya kesi 20 ziliamuliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania na asilimia 90 ya watuhumiwa walitiwa hatiani wakipewa adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka 20 hadi kifungo cha maisha.


Kwa mahakama za chini jumla ya watuhumiwa 343 walitiwa hatiani, 65 waliachiwa huru na hadi taarifa hiyo inatolewa kesi 1,378 zilikuwa katika hatua ya usikilizwaji.


Kifo njenje


Kwa mujibu wa kamishna huyo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya akili na dawa za kulevya, kuna athari nyingi za kiafya zinazosababishwa na matumizi ya dawa hizo huchangia mishipa ya damu kupasuka, kupata kiharusi, kutokwa na damu puani na vifo vya ghafla ambavyo husababishwa na kuchanganya aina mbalimbali za dawa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad