Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewaeleza wabunge katika chama chake cha kihafidhina kuwa anategemea vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona vitadumu hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili.
Kulingana na gazeti la kila siku la hapa Ujerumani la Bild, Merkel amesema kwamba endapo watashindwa kukabiliana na aina mpya ya virusi vilivyogunduliwa Uingereza, basi kunaweza kuwepo na maambukizi mara kumi kufikia hadi sikukuu za Pasaka.
Ujerumani imezidisha hatua za nchi nzima na kupanua kufungwa kwa shughuli za umma hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. Hadi kufikia leo Jumanne, taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya Robert Koch imesajili visa vipya elfu 12,802 vya COVID-19.
Wakati huohuo waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Soeder ametaka mjadala wa kuanzishwa chanjo za lazima kwa wahudumu wa nyumba za kutunza wazee.
@