Miili ya watu yapatikana pwani ajali ya ndege Indenesia




Nchini Indonesia, sehemu za miili ya watu waliohusika kwenye pwani ya ndege zimeopolewa katika kisiwa cha Jakarta Mahala ambapo ndege iliyokuwa imebeba abiria 62 ilianguka muda mfupi baada ya kuruka.
Msemaji wa polisi Yusri Yunus amesema, leo Jumapili asubuhi, kuwa wamepokea mifuko miwili mmoja ukiwa na sehemu hizo za mwili na mwingine ukiwa na mali zinazoaminika kuwa ni za abiria.

Mamlaka nchini Indonesia imesema rada ya kufwatilia ndege inaonyesha kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 737-500 ilianguka baharini takriban dakika nne baada ya kuondoka kutoka kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Soekarno-Hatta mjini Jakarta. Ilikuwa inaelekea kwenye mji wa Pontianak ulio katika kisiwa cha Borneo. Safari ya ndege hiyo ilitegemewa kuchukua muda wa dakika 90 juu ya usawa wa bahari ya Java.

Waziri wa uchukuzi wa Indonesia Budi Karya Sumadi amewaambia waandishi wa habari kuwa ndani ya ndege hiyo walikuwemo watu hao 62 miongoni mwao wahudumu wa ndege pamoja na watoto 10.

Waziri Sumadi amesema ndege hiyo ilichelewa kwa saa moja kabla ya kuruka na ilipoondoka mwendo wa saa nane na dakika 36, dakika nne baadaye, ikapotea kutoka kwenye Rada baada ya rubani kutoa mawasiliano kwa kitengo cha udhibiti wa safari za anga kuwa anaruka umbali wa futi 29,000 usawa wa bahari.

Eneo linalodhaniwa kutokea ajali hiyo ya ndege ni karibu na visiwa maarufu vinavyotembelewa na watalii kando na pwani ya mji mkuu wa Indonesia, Jakarta.

Wavuvi katika eneo lililo karibu na mlolongo wa visiwa kaskazini mwa pwani ya Jakarta, waliripoti baada ya kusikia mlipuko mwendo wa saa nane na nusu mchana siku ya Jumamosi. Mvuvi mmoja ameliambia shirika la habari la AP kwamba waliposikia mlipuko huo walidhani labda ni bomu au Tsunami na baada ya hapo waliuona mlipuko mkubwa kutoka baharini.

Mamlaka imeweka vituo viwili vya kushughulikia yanayohusiana na ajali hiyo, kimoja kwenye uwanja wa ndege na kingine kipo bandarini. Familia zimekusanyika katika vituo hivyo kusubiri taarifa za wapendwa wao.

Kwenye mitandao ya kijamii, watu walianza kuzungusha taarifa za ndege hiyo nambari SJ-182 ya shirika la ndege la Sriwijaya Air, picha na video za watu waliorodheshwa kama abiria kwenye ndege hiyo. Moja kati ya video hizo inamwonyesha mwanamke na watoto wake wakipunga mikono ya kwaheri katika uwanja wa ndege kabla ya kuondoka.

Mkurugenzi wa shirika hilo la Sriwijaya, Jefferson Irwin Jauwena amewaambia waandishi wa habari kwamba ndege hiyo iliyohudumu kwa miaka 26 hapo awali ilitumiwa na mashirika ya ndege ya Marekani, haikuwa na matatizo yoyote na kwamba kabla ya kupata ajali siku hiyo hiyo ilikuwa tayari imefanya safari kwenda katika miji ya Pontianak na Pangkal Pinang.

Indonesia, taifa lenye watu milioni 260 inayosifika kuwa na idadi kubwa ya visiwa duniani mara kwa mara  imekumbwa na ajali zinazohusisha vyombo vya usafirishaji wa ardhini, baharini na angani. Inadaiwa ni kutokana na miundo mbinu chakavu na viwango duni vya usalama katika sekta ya usafiri.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad