KIASI cha shilingi milioni 50, ndicho kinachotajwa kuwa thamani ya beki wa kati wa Polisi Tanzania, Iddy Mobby ambaye ameonesha nia ya kujiunga na Yanga kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Beki huyo ambaye anatajwa na Yanga kwa muda mrefu, hivi sasa yupo kwenye mazungumzo na viongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kumsajili.
Meneja wa mchezaji huyo, Joseph Assey, amesema thamani ya mkataba wa mchezaji huyo siyo chini ya shilingi milioni 50, hivyo timu yoyote ambayo itamhitaji itatakiwa kutoa kiasi hicho.
Akizungumza na Spoti Xtra, Assey alisema, beki huyo bado ana mkataba wa miezi saba na Polisi Tanzania.“Thamani ya Mobby ni shilingi milioni 50 na siyo chini ya hapo, kama kuna timu yoyote itakuwa inahitaji huduma yake inatakiwa itoe mshiko huo.
“Wengi wanazungumza kuhusu Yanga, kweli huo mpango upo ingawa siyo rasmi sana na siwezi kuzungumzia sana kwa sababu bado ana mkataba wa miezi saba na Polisi Tanzania,” alisema Assey.
Alipotafutwa Iddy Mobby kuzungumzia hilo, alisema: “Kwa sasa sitaki kuzungumzia ishu za kwenda Yanga, hizo ishu zipo ila ninachofahamu kwa sasa mimi ni mchezaji wa Polisi Tanzania.”
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema anahitaji nyota watatu ili kukamilisha usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa Januari 15, mwaka huu.
Nafasi ambazo Yanga inahitaji kusajili ni pamoja na mshambuliaji ambaye anayetajwa kutua ni Ferebory Dore raia wa Congo Brazzaville, kiungo na beki wa kati ambaye anayehusishwa zaidi ni Iddy Mobby.
Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said, alisema kabla usajili haujafungwa Januari 15, mwaka huu, watatangaza wachezaji wao wapya wakiwemo wazawa wawili.