Mlanguzi mkubwa wa mihadarati Asia amekamatwa Amsterdam




Polisi nchini Uholanzi wamemkamata anayesemekana kuwa kiongozi wa genge moja kubwa la ulanguzi wa mihadarati duniani, baada ya Australia kutoa kibali cha kukamatwa kwake.

Tse Chi Lop - Raia wa Canada mwenye asili ya China - inasemekana kuwa yeye ndio kiongozi wa genge hilo, ambalo linamiliki karibu dola bilioni 70 la soko haramu la dawa za kulevya kote barani Asia.

Akiorodheshwa kama mmoja wa watoro wanaotafutwa, Bwana Tse alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Schiphol, Amsterdam.

Sasa Australia itataka ahamishwe hadi nchini humo kukabiliana na mkono wa sheria.

Polisi nchini Australia inaamini kuwa kampuni ya mlanguzi huyo ambayo pia inafahamika kama Sam Gor Syndicate, ndio inayoingiza hadi asilimia 70 ya mihadarati nchini humo.

Mlanguzi huyo, 56, amekuwa akilinganishwa na mlanguzi wa Mexico Joaquin "El Chapo" Guzman kwasababu ya ukubwa wa biashara yake haramu anayoendesha.

Polisi nchini Australia inasemekana kwamba imekuwa ikimtafuta Bwana Tse kwa zaidi ya miaka kumi kabla ya kukamatwa Ijumaa wakati akiwa anasubiri kuingia ndege ya kwenda Canada.

Taarifa ya polisi ambayo haikutaja jina la Bwana Tse, ilisema kibali cha kukamatwa kwake kilitolewa 2019, huku polisi nchini Uholanzi wakifanyia kazi taarifa iliyotolewa na Interpol.

"Alikuwa kwenye orodha ya wanaotafutwa na alikuwa anazuiliwa kulingana na taarifa za shirika la ujasusi," Msemaji wa polisi Uholanzi amesema Ijumaa.

Shirika la habari la Reuters lilichapisha uchunguzi maalum kuhusu Bwana Tse mwaka 2019 - na kumuelezea kama "Mtu anayetafutwa zaidi Asia".

Shirika hilo lilinukuu makadirio ya UN yalionesha kwamba mapato ya genge hilo kutokana na uuzaji wa dawa ya methamphetamine pekee huenda ni dola bilioni 17 mwaka 2018.

Juhudi za kumkamata Bwana Tse, zilijumuisha mashirika karibu 20 ya mabara mbalimbali duniani huku lile la AFP likishika usukani, kulingana na shirika la Reuters.

Ilisemekana kwamba miaka ya karibuni Bwana Tse amekuwa akiendesha shughuli zake katika miji ya Macau, Hong Kong na Taiwan.

Awali, alitumikia kifungo cha miaka 9 gerezani baada ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Marekani miaka 1990.

Vyombo vya habari vya Australia vimeelezea kukamatwa kwake kama "muhimu zaidi" kwa kikosi cha polisi nchini humo katika kipindi cha miaka 20.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad