Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya amewataka wafanyabiashara waliotoa stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kisha zikabandikwa kwenye pombe kali bandia, wajiandae kisaikolojia.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake, Sabaya amesema mfanyabiashara yeyote au mmiliki wa kiwanda anayefahamu alishiriki kutoa stika hizo zikatumika kuhujumu uchumi, wajisalimishe wenyewe TRA.
Sabaya amesema tayari ameiagiza TRA kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mnyororo wote uliohusisha stika hizo hadi wafikie mahali ambapo mzizi wake upo.
Usiku wa kuamkia Januari 20,2021, mkuu huyo wa wilaya akiwa na maofisa wa TRA, Polisi na Takukuru, walifanya ukaguzi wa kushtukiza katika duka moja na kudai kubaini ukwepaji wa kodi za serikali.
Pia katika upekuzi sehemu ya nyuma ya duka hilo la rejareja, kulikutwa katoni za pombe kali mbalimbali na siku iliyofuata upekuzi ulibaini katoni nyingine karibu 200 za pombe zinazodaiwa ni feki zikiwa na stika hizo.
Usiku huo huo, DC Sabaya aliagiza kukamatwa kwa mmiliki wa duka hilo na mkewe na duka hilo lililokuwa na bidhaa zinazodaiwa za jumla, liliwekwa chini ya ulinzi na upekuzi na ukaguzi ukaendelea kwa saa zaidi ya 48.
“Nimewaagiza TRA na Takukuru wakikuta stika iliyopaswa kuwa kiwanda C iko kiwanda A waende mpaka kule mwanzo wagundue stika zilizokaje kwenye kiwanda chao, nani alizitoa na nani alizisambaza,” amesema Sabaya.
“Lakini hata huyu (anayedaiwa kukutwa na pombe bandia) atatuambia hizi pombe feki zinatengenezwa wapi na nani na nani ana suppy (kusambaza) hizo stika za TRA tulizozikuta kwenye hizi pombe,” amesisitiza Sabaya.
Sabaya alidai tangu juzi na jana, mfanyabiashara huyo amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi ni kwamba tayari ameanza kuwataja wafanyabiashara wengi kwa idadi, aliokuwa akishirikiana nao.
“Kwa sababu kwa container zilizokuwapo pale huyu mtu (mfanyabiashara) anafahamiana na huyo mfanyabiashara au kiwanda kinachozalisha pombe hizo. Tutafukua na nawaambia hakuna jiwe halitaguswa.”
“Wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika sana kuhusu kushuka kwa biashara, lakini sisi sasa tunaanza kupata mashaka hii ndio aina mpya ya biashara ambayo imezuka wanaifanya hapa kwetu.”
“Kwa sababu yule mtu amewataja wafanyabiashara wengi ambao alikuwa akishirikiana nao. Imeonekana kuna baadhi ya maeneo walikuwa wanachukua bidhaa, lakini kule anapochukua hapewi risiti.”
Kwa mujibu wa Sabaya, katika uchunguzi wa awali imebainika baadhi ya pombe anazodai ni za bandia zilikuwa zimefichwa katikati ya mifuko ya mbolea na stika za TRA zilizokutwa zilikuwa hazioani.
“Tukagundua duka lingine la Agrovet na ndani tukakuta pombe ambazo kwanza ni bandia lakini stemu za TRA zina mismatch (hazioani). Kwa mfano stika ya maji inakutwa kwenye hizo pombe kali feki”.
“Moja tumekubaliana kwamba Takukuru waendelee na kazi yao na TRA ku kubaini kodi halali ya serikali iliyokwepwa. Lakini tumekubaliana pia TRA na Takukuru wachimbe kwa kina hili la stika za mamlaka ya kodi.”
Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi, alipoulizwa na kuhusiana na uchunguzi huo wa Stika za TRA zilizokutwa kwenye pombe zinazodaiwa ni feki alisema hataweza kulizungumzia kwa kuwa anaumwa.
Ingawa Meneja wa mkoa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu za kiafya, lakini operesheni na uchunguzi huo unamhusisha kaimu Meneja wa TRA wilaya ya Hai, Jullius Sanare na wengine kutoka mkoani.