Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga amesema wataendelea na msakao wa watu wanaowatumia walemavu katika vitendo vya kuwadhahlilisha mpaka watakapo hakikisha wahusika wanofanya vitendo hivyo wanaacha kabisa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (katikati) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Shinyanga, Ndg. Richard Mpongo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Yasinta Mboneko.
Ummy amesema hayo wakati wa ziara yake ya kuwarejesha baadhi ya watu wenye ulemavu karibu 38 mkoani Shinyanga kutoka Jijini Dar es Salaam, kutokana na kundi hilo kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi kuwazungusha watu wenye ulemavu kuomba fedha barabarani.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Yasinta Mboneko (kulia) akieleza jambo wakati wa kikao hicho. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (pembeni) ni Katibu wa Naibu Waziri huyo Bw. Omary Sama
“Leo hii tumewarejesha Watu wenye Ulemavu zaidi ya 38 kutoka Jijini Dar es Salaam kuja hapa Mkoani Shinyanga mahali ambapo wamekuwa wakiishi hapo awali, hivyo kama rejista hiyo ingekuwepo basi zoezi la utambuzi wa baadhi yao ingekuwa rahisi kuwatambua, Tutaendelea na msako hadi pale tutakapoona wahusika wa mtandao huu wanaacha kabisa vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu,” alisisitiza Naibu Waziri Ummy
Aidha Naibu Ummy ameeleza serikali ipo katika mkakati wa kuandaa regista ya watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Halmashauri na Mkoa ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoonyesha idadi ya wenye ulemavu ,kujua mahali walipo, wanajishughulisha na nini katika jamii waliyopo.
“Uwepo wa rejista hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa serikali kutambua idadi ya watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo mbalimbali na hivyo kurahisisha ufikikaji wa huduma kwa kundi hilo kwa urahisi,” alisema Naibu Waziri Ummy