MSHAMBULIAJI wa Klabu ya Yanga, Fiston Abdulazack ambaye ni mtambo wa mabao leo Januari 29 amewasili rasmi ndani ya ardhi ya Bongo ili kujiunga na timu hiyo.
Raia huyo wa Burundi ni ingizo jipya kwenye usajili wa dirisha dogo ambao umefungwa Januari 15,2021 baada ya kufunguliwa Desemba 16,2020.
Ni chaguo la Kocha Mkuu, Cedric Kaze ambaye amekuwa akipata tabu kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Michael Sarpong, raia wa Ghana mwenye mabao manne ndani ya Ligi Kuu Bara.
Aliweza kufanya vizuri na timu yake ya Taifa ya Burundi kwenye michuano ya Afcon ambapo aliweza kuwa mmoja ya washambuliaji ambao walitupia mabao sita jambo ambalo limekuwa likimuongezea thamani.
Amepokelewa na viongozi wa Yanga wakiongozwa na Injinia Hersi Said ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili ndani ya Yanga pia ni Mkurugenzi ndani ya Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa timu hiyo.
Mashabiki wa Yanga pia walijitokeza kwa wingi wakiongozwa na Ofisa Muhamasishaji, Antonio Nugaz mzee wa wape salamu.
Fiston amesema kuwa atafanya vizuri kwa kuwa kazi yake ni mpira hivyo mashabiki wampe sapoti naye hatawaangusha.
Nyota huyo amesaini dili la miezi sita ambalo lina kipengele cha kuongeza mkataba ikiwa atafanya vizuri ndani ya kikosi hicho.