Muuguzi adaiwa kumzaba makofi mwanamke aliyejifungulia sakafuni




 

Muuguzi wa zamu katika Kituo cha Afya Mazwi mjini Sumbwanga anadaiwa kumzaba makofi usoni mwanamke mmoja aliyejifungulia sakafuni kwenye moja ya vyumba vya kituo hicho juzi usiku.


Taarifa zilizopatikana kutoka kwenye kituo hicho, zinasema mama huyo ambaye jina lake halijawekwa hadharani, alifika hapo kujifungua na kitendo cha kujifungulia sakafuni kilimkera muuguzi huyo.



Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbwanga, Jacob Mtalitinya alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa tayari wamemsimamisha kazi muuguzi huyo aliyemtaja kwa jina la Valentine Kinyaga ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.



Shuhuda wa tukio hilo, ambaye hakutaka atajwe gazetini alieleza kuwa mjamzito huyo alifika kwenye kituo hicho cha afya cha Mazwi yapata saa 7.00 usiku.



Alipofika kwenye kituo hicho, taarifa zinaeleza alifuata taratibu za kawaida za kuonana na watu wa mapokezi na wauguzi waliokuwa hapo.



Mama huyo inadaiwa alipokewa na muuguzi huyo aliyekuwa zamu na kupelekwa chumba maalumu kwa ajili ya kusubiri kujifungua.



“Baada ya kufika kwenye chumba hicho, inadaiwa muuguzi huyo alimwelekeza asubiri kuhudumiwa.



“Ila sasa baada ya kuwa amewekwa kwenye chumba hicho, muuguzi aliondoka,” anasimulia shuhuda, ambaye alikwenda hapo kwa matibabu na kushuhudia mkasa huo.

 

Habari zaidi zinadai kwamba, baadaye mjamzito huyo alianza kulalamika amebanwa na uchungu lakini muuguzi huyo alipokwenda tenda chumbani humo alimtaka aendelee kusubiri.



“Wakati mama huyo anaendelea kusubiri, ilifika hatua ya kujifungua na akatandika kanga yake sakafuni na kujifungua.



Inaelezwa kuwa baada ya kujifungua, wanawake waliokuwa katika chumba hicho wakisubiri kujifungua walimuita muuguzi huyo wa zamu na kukuta mama huyo amejifungulia sakafuni.



Hata hivyo, baada ya kupewa taarifa ile, muuguzi huyo alianza kuhamaki kwa hasira kutokana na kuchukukizwa na kitendo cha mama huyo kujifungulia kwenye sakafu ya hospitali ile.

 

Muuguzi huyo inadaiwa alianza kumpiga makofi mama huyo huku akimfokea kwanini amejifungulia sakafuni pasipo kumtaarifu yeye ili ampeleke chumba cha kujifungulia.



“Muuguzi alikuwa mkali hasira zilimpanda zaidia akampiga makofi usoni yule mama,” alieleza shuhuda yule.



Shuhuda huyo anadai baada ya kumpiga makofi, ndipo alianza kumsaidia kwa kumtoa mtoto na kuendelea kumpa huduma.



Kitendo cha mama huyo kupigwa makofi na muuguzi kiliwaudhi sana ndugu zake waliokuwa wakimsubiri ajifungue.



Inadaiwa walitoa taarifa kwa uongozi wa hospitali hiyo, ambapo ulipeleka taarifa katika mamlaka za juu za kiutawala wa hospitali hiyo ili uchukue hatua stahiki.



Kufuatia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbwanga, Mtalitinya alisema wamemsimamisha kazi muuguzi hiyo ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.



Alipoulizwa kama atachukuliwa hatua za kisheria, Mtalitinya alieleza kuwa hatua yao ya kwanza ni kufanya uchunguzi.



Mtalitinya alisema kwa upande wake madaraka yake yanaishia katika kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishii huyo, ila sasa aliyefanyiwa kitendo hicho ana uhuru wa kuamua kama atataka kuchukua hatua za kisheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad