Mwanamke alivyouawa na mchunga ng’ombe wake akitaka kurithi mali




Antonia Jitinde (62) aliyeishi katika kijiji cha Zawa, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, hakuwahi kuhisi kuwa ngo’mbe 25 na shamba alilomiliki siku moja vingegeuka chanzo cha maisha yake kutatishwa kinyama na mtumishi aliyetaka kurithi mali zake.


Bibi huyu ambaye hakuwa na mtoto aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga Oktoba 2013 na John Shini (33), kijana aliyemwajiri kwa miaka mingi kuchunga ng’ombe wake.



Kutoonekana kwa bibi huyo kwa siku kadhaa baada ya kuuawa na kuzikwa kwenye shimo lisilotumika kuliibua wasiwasi mkubwa kwa majira na ndugu zake.



Shini aliamini kazi imekwisha na kwamba baada ya kumzika bosi wake waliyeishi nyumba moja, mali za marehemu zingekuwa zake. Mambo hayakuwa hiyo.



Damu ya Jitinde haikumwacha Shini Salama. Haikutaka kupotea bure.



Kwa miaka kadhaa, Jintinde aliamua kuishi maisha ya peke yake kwa kuwa alikuwa hakujaliwa kupata mtoto. Wakati akiendelea na maisha yake aliamua kumwajiri John Shini, ili amsaidie kuchunga ng’ombe wake.



Aliishi na Shini kwa miaka mingi kabla ya kupotea ghafla kwenye macho ya watu mwanzoni mwa mwezi Oktoba, mwaka 2013.



Wakati majirani na wanakijiji wenzake wakijiuliza bibi huyo alikuwa wapi, Shini alionekana akiendelea na shughuli zake za kuwapeleka ng’ombe malishoni na kuwarudisha kama kawaida.



Hali ya kutoonekana kwa bibi huyo iliibua wasiwasi miongoni mwa majirani na wanakijiji wenzake. Wasiwasi ulizidi pale Shini alipoonekana akiuza ng’ombe wa mwajiri wake kwa bei ya kutupa, bila wasiwasi wowote.



Minong’ono ikazidi kijijini pale. Hali hiyo ilimfanya mgambo wa kijiji, Sagani Peter kwenda kumweleza mwenyekiti wa kijiji, Mohamed Ziraimu kuhusu wasiwasi wa kupotea bibi huyo.



Baada ya kumsikiliza Peter, kiongozi huyo wa kijiji alimwamuru aende moja kwa moja kumkamata Shini.



Oktoba 28, 2013 Shini alikamatwa na kupelekwa kwa mwenyekiti wa kijiji kuhojiwa kama anafahamu lolote kuhusu kutoweka kwa bosi wake.



Wakati wa mahojiano, aliwaeleza viongozi wa kijiji kuwa bibi huyo alimuaga kuwa anakwenda katika kijiji cha Isoro kutafuta dawa ya kienyeji ijulikanayo kwa kisukuma kama ‘kiziba’ ili imsaidie kuwalinda ng’ombe wake dhidi ya wezi.



Alipoulizwa imekuwaje ameanza kuuza ng’ombe wake, Shini alisema bosi wake alimwagiza auze baadhi ya ng’ombe ili apate fedha za kununulia dawa.



Majibu yake hayakuwaridhisha wachunguzi na ndipo walipoamua kumpeleka kituo cha Polisi Shishiwi kwa mahojiano zaidi.



Hata hivyo, polisi katika kituo hicho walimwachia baada ya muda mfupi, wakidai hakukuwa na malalamiko ya kupotea mtu yaliyoripotiwa kwao.



Siku moja baada ya Shini kuachiwa na polisi, mwenyekiti wa kijiji alimwelekeza tena mgambo Peter kumkamata Shini kwa kuwa ndugu wa bibi huyo tayari walisharipoti polisi kutoonekana kwake.



Akiri kumwua bibi

Baada ya kukamatwa mara ya pili, kabla ya kupelekwa polisi, hatimaye Shini alikiri mbele ya kiongozi wa kijiji kuwa yeye ndiye alimwua bosi wake kwa sababu alitaka kurithi ng’ombe na shamba lake.



Aliwaambia kuwa alitekeleza mauaji hayo kwa kushirikiana na rafiki zake Tungu Malambi na Charles Makomango.



Kutokana na kukiri kwake, viongozi wa kijiji waliamua kuwaita polisi wamchukue mtuhumiwa. Baada ya askari kufika, Shini alikiri kwa mara ya pili mbele ya wazee wa kijiji, mwenyekiti wa kijiji na diwani kuwa ndiye aliyemuua bosi wake kwa tamaa ya kutaka kurithi mali.



Aonesha alipomzika

Siku iliyofuata (tarehe 30 Oktoba, 2013), Shini aliwaongoza polisi na viongozi wengine wa kijiji hadi kwenye nyumba ya marehemu na kuwaonyesha shimo alimomzika. Marehemu alilitumia shimo hilo kuchimba udongo wa kutengenezea matofali.



Kundi la wanakijiji ambao walikusanyika kwa wingi kufuatilia mbiu ijulikanayo kwa kisukuma ‘mwano’, kwa kushirikiana na polisi waliokuwa na amri ya mahakama ya kufukua mwili walianza kazi hiyo mara moja.



Haukupita muda, mwili wa Jitindee ulionekana ukiwa umeharibika. Mwili huo ulitambulika kwa blauzi nyeusi na sketi ya udhurungi alizopendelea kuvaa wakati wa uhai wake.



Baada ya kazi ya kufukua na kutambua mwili iliyoongozwa na daktari Nyagala kukamilika, polisi waliruhusu ndugu wa marehemu kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi.



Hapo Shini na washukiwa wenzake wawili walikamatwa, lakini baadae marafiki waliachiwa kwa kukosekana ushahidi dhidi yao.



Ashtakiwa

Shini alishtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia mwaka 2013. Alipotakiwa kujibu shtaka, Shini hakukana kutenda kosa.



Alipohojiwa na wakili wa Serikali, mshtakiwa huyo alieleza kuwa alimfahamu marehemu kama jirani yake aliyeishi peke yake na kwamba alimiliki ng’ombe 20.



Mwaka 2016 Jaji wa Mahakama Kuu Shinyanga, Victoria Makani alimhukumu Shini adhabu ya kunyongwa hadi kufa, akitumia zaidi ushahidi wa mazingira na kukiri kwake kosa kwa maneo kwa viongozi wa kijijij na polisi kulikosababisha kupatikana kwa mwili wa marehemu.



Jaji alisema pia uamuzi wake ulizingatia taarifa ya onyo ambamo mshtakiwa alieleza kwa kirefu jinsi alivyoshiriki katika mauaji.



Akata rufaa

Shini hakuridhishwa na adhabu hiyo na mwaka 2016 alikata rufaaa yenye sababu saba kwa nini anapinga hukumu dhidi yake.



Hata hivyo, Agost 5, 2020 wakili aliyemtetea, Paul Kaunda aliwasilisha upya sababu nne tu za rufaa.



Katika hoja ya kwanza, alidai kuwa mahakama ilikosea kumhukumu kifo kwa kuzingatia ushahidi wa mgambo, mwenyekiti wa kijiji, mnunuzi wa ng’ombe na askari mpelelezi ambao ulikuwa haujaungwa mkono na ushahidi mwingine.



Alidai kati ya hao hakuna aliyetoa ushahidi kuwa alimwona mrufani akimwua marehemu.



Alidai pia mahakama ilikosea kwa kutegemea ushahidi wa kikiri kwake kwa mdomo na pia kutozingatia ushahidi wa taarifa yake ya onyo unaomtoa kwenye hatia ya kuua.



Wakili Kaunda alisema Mahakama Kuu haikupaswa kuzingatia uliodaiwa ushahidi wa mshtakiwa kikiri kosa kwa mdomo mbele ya viongozi wa kijiji na mgambo bila kuthibitisha kuwa kukiri huko kulifanyika kwa hiari. Alidai kukiri huku kulifanywa kinyume na utaratibu wa kisheria na kwa vitisho.



Alionyesha wasiwasi wake kwa nini upande wa mashtaka hawakuwaita ndugu wa marehemu kutoa ushahidi mahakamani.



Katika rufaa hiyo, Jamhuri iliwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga aliyesaidiana na mawakili wa Serikali Salome Mbughuni, Caroline Mushi na Immaculata Mapunda.



Majaji watupa rufaa

Ikitoa hukumu yake Agosti mwaka jana, Mahakama ya Rufani ilisema hakukuwa na shaka kuwa kesi dhidi ya Shini kwa kiasi kikubwa kwenya ushahidi wa kimazingira kwa kuwa hakukuwa na aliyeshuhudia wakati kosa hilo likitendeka.



Majaji wa Mahakamaya Rufani---Augustino Mwarija, Jacobs Mwambegele na Rehema Kerefu walieleza kuwa ushahidi uliotumika na mahakama iliyomhukumu ilikuwa ni taarifa ya kukiri kosa kwa mdomo mbele ya viongozi wa kijiji na mgambo ambao hatimaye uliowezesha kupatikana mwili wa marehemu.



Pili, walizingatia ushahidi wa mtu aliyenunua ng’ombe toka kwa mrufani na tatu, taarifa yake ya ambayo ameeleza kwa kirefu jinsi marehemu alivyouawa na kuzikwa na nafasi yake katika mchakato wa kumuua.



“Ni maoni yetu, kama ilivyoonekana pia na mahakama iliyomhukumu, kwamba maelezo haya yote yanatoa ushahidi wa kutosha wa ushiriki wa mrufani katika kutenda kosa. Mazingira na maelezo yaliyosababisha kugunduliwa kwa mwili wa marehemu yanatosha kuthibitisha mrufani alishiriki katika kumuua marehemu,” walisema majaji hao.



Majaji hao walisema kuwa kukiri kosa kwa mshtakiwa mbele ya viongozi wa kijiji, mgambo na polisi kulikuwa na umuhimu wa pekee kwa sababu hatimaye uliwezesha kupatikana mwili wa marehemu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad