Kulia ni mtu aliyedhaniwa kuwa ni mwigizaji Chuck Norris.
MENEJA wa mwigizaji na msanii wa michezo ya viungo maarufu, Chuck Norris, amelazimika kukanusha kwamba nyota huyo alikuwepo katika mashambulizi yaliyofanyika katika Bunge la Marekani (Capitol Hill) wiki iliyopita baada ya picha moja kumwonyesha mtu mmoja ambaye anafanana naye ambayo ilitolewa katika mitandao ya kijamii.
Norris (80) pia alituma ujumbe katika mitandao ya kijamii akipinga hakuwepo kwenye mashambulizi hayo.
Baada ya vurugu hizo, picha moja ilitolewa na mfuasi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ikiomwonyesha mtu huyo aliyefanana na mwigizaji huyo.
Picha hiyo ilisababisha tafrani ambapo watu wengi walioiona mtandaoni waliamini ndiye nyota huyo.
Mwigizaji na msanii wa michezo ya viungo maarufu, Chuck Norris.
Akizungumza jana (Jumanne) meneja wa msanii huyo, Erik Kritzer, alithibitisha kwamba mtu aliyekuwa katika picha hiyo si Chuck Norris.
Naye Chuck Norris, katika ujumbe wake mtandaoni aliandika:
“Nimegundua kwamba kwa bahati mbaya kulikuwa na mtu anayefanana na Chuck Norris kwenye mashambulizi yaliyofanyika Bungeni (DC Capitol) Januari 6. Mtu huyo hakuwa mimi na sikuwepo.
“Nataka kusema wazi kwamba hapana nafasi ya vurugu za aina yoyote katika jamii yetu, ikiwa ni pamoja na maandamano ya kisiasa na kwamba kukabidhiana madaraka ni jambo la msingi kwa mfumo wetu wa kidemokrasia wa serikali. Ninaheshimu na nitaheshimu Sheria naTaratibu zilizopo.
“Rafiki yenu, Chuck Norris.”
Naye meneja wake alisema: “Chuck yuko nyumbani kwake huko Texas na familia yake na yeye ana sura nzuri zaidi ya yule aliyeko kwenye picha.”