Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema viongozi wote wa sekta za umma na binafsi wanatakiwa waendelezwe kitaaluma kwa ajili ya kukuza weledi, ubunifu na maadili ili waweze kusimamia ipasavyo maendeleo na kuongeza tija na mapato ya Taifa.
Amesema katika kipindi hiki ambacho nchi imeingia katika uchumi wa kati, serikali ingependa kuona nguvukazi katika ngazi mbalimbali inaimarishwa na kuhakikisha viongozi wanatumia ujuzi na weledi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miradi.
"Dhana ya uanagenzi ni suluhisho la kuhakikisha wataalamu wetu wanajengewa ujuzi unaohitajika mara kwa mara ili kuwaongezea umahiri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, nchi inahitaji viongozi wanaoongoza kwa vitendo na kuwa mfano bora kwa Taifa", amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema kuwa manufaa na faida za kuwajengea uwezo wataalam wa ndani hususani viongozi na maafisa watendaji wakuu ni pamoja uwepo wa rasilimali na nguvu kazi ya Taifa yenye ubora wa ujuzi, weledi na umahiri wa hali ya juu unaowawezesha kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema manufaa mengine ni nchi kuwa na viongozi na watendaji wakuu wabunifu, wenye maadili na uzalendo ambao wapo tayari kujenga uchumi imara, endelevu na unaokua pamoja na kukuza uwezo wa kitaalam na ujuzi wa matumizi ya teknolojia mpya ya kidijitali.