NEC yajibu vikwazo vya Marekani



Dar es Salaam. Wakati Marekani ikitangaza kuweka vikwazo kwa baadhi ya maofisa wa Serikali ya Tanzania kwa madai ya kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imejibu madai hayo ikisema zipo sheria za kufuata kama kuna kasoro.


Taarifa ya kusudio la kuweka vikwazo vya visa kwa Watanzania imetolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo aliyeandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema ni kutokana na vitendo vya kuingiliwa kwa uchaguzi huo.

 

“Kuna matokeo ya kuingilia mchakato wa kidemokrasia. Kuanzia leo (juzi), tunaweka vikwazo vya visa kwa wale waliohusika kuingilia uchaguzi nchini Tanzania. Tunaendelea kufanya kazi kuendeleza demokrasua na mafanikio ya pamoja kwa nchi zetu mbili,” umesomeka ujumbe wa Pompeo katika Twitter.


Hata hivyo, taarifa ya Pompeo iliyotolewa Januari 19 katika tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, haijataja maofisa wanaolengwa na vikwazo hivyo, lakini inafuatilia kwa karibu mwenendo wa demokrasia na haitasita kuchukua hatua zaidi.


Kwa upande wake Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela alipoulizwa kwa simu kuhusu taarifa hiyo alisema hawajaipata rasmi

 

“Hatujapata taarifa rasmi zaidi ya kuona katika mitandao na hatuwezi kufanyia kazi vitu vya mitandaoni. Wizara yetu ina utaratibu mzuri wa mawasiliano na Balozi na hatujaletewa taarifa rasmi,” alisema Buhohela.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema taarifa hiyo haijafafanua kinacholalamikiwa na sheria za Tanzania zinaelekeza kupeleka mashitaka mahakamani pale mlalamikaji anapoona sheria hazikufuatwa.


“Hayo ni maoni yao, sasa Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi atafanya nini? Waeleze basi huo uchaguzi uliingiliwaje? Maelezo yao hayajaeleweka bado,” alisema.


Jaji Kaijage aliyesema kwa sasa yuko likizo, alisema katika uchaguzi huo kulikuwa na waangalizi na walitoa ripoti zao za awali na wameendelea kutoa ripoti kuu.


“Kulikuwa na accredited observers (waangalizi waliopewa vibali) na walitoa ripoti. Tuone walisemaje kwenye ripoti zao. Kama Marekani walikuwa na waangalizi ripoti yao itaonyesha. Kwa sasa mimi niko likizo sijaona ripoti walizotoa.


Aliendelea kufafanua; “Unaposema uchaguzi umeingiliwa inakuwa ni general statement kauli ya jumla). Ni lazima useme umeingiliwa kivipi? sio sweeping statement. Sheria zetu ziko wazi kama unaona kuna kasoro baada ya uchaguzi unafanya uchunguzi wa kisheria uone kama kuna makosa labda katika uteuzi wa wagombea au wakati wa kupiga kura. Baada ya hapo unakwenda mahakamani kushitaki.”


Alipoulizwa kuhusu vikwazo hivyo alisema: “Issue sio mara ya kwanza au ya pili kuwekewa vikwazo, ila ni basis (msingi) ya hivyo vikwazo. Aulizwe yeye aliyechukua hatua na sio sisi. Lakini statement yao iko too general, haiko concrete.”


Katika tovuti ya Serikali ya Marekani umetolewa ufafanuzi wa kauli ya Pompeo ikisema vitendo vilivyofanywa na maofisa wanaotuhumiwa ni mwendelezo wa ukandamizaji wa demokrasia.


“Waangalizi wa uchaguzi na asasi za kiraia zilishuhudia ukandamizaji na uvunjifu wa haki za binadamu, kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Wagombea wa upinzani walienguliwa, wananyanyaswa na kukamatwa.


“Kuongezeka kwa kasoro za upigaji kura, kufungwa kwa intaneti, manyanyaso kwa waandishi wa habari na vurugu zilizosababishwa na vyombo vya usalama vyote viliufanya uchaguzi huo usiwe huru wala wa haki. Viongozi wa asasi za kiraia walipata vitisho na wa upinzani wamekimbia nchi wakihofia usalama wao,” imesema taarifa hiyo.


Marekani imeitaka Serikali ya Tanzania kuchunguza na kuwachukulia hatua waliohusika na makosa ya uchaguzi na vurugu


Hii si mara ya kwanza kwa Marekani kuweka vikwazo vya visa kwa watendaji wa Serikali ya Tanzania. Januari 31, 2020, Pompeo alitangaza kumpiga marufuku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mkewe kuingia nchini humo kwa madai ya uvunjifu wa haki za binadamu.

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Akaunti ille ya twita ni ya kutengenezwa na Vijana wa Kichedemu.
    Serikali iliyoondoka madarakani na aibu nyingi ina yake na sisi tuna yetu

    Kila mmoja aangalie yake. Tuheshimiane.

    Twita na tokotoko na shangazi yake fwezibuku wote na dada swetiglamu wote
    ni Wananchi wa Mwita Dao. sasa basi sisi ni wananchi wa Duniani vitu 2 tofauti.

    NEC NA WATANZANIA. WAPIGA KELELE NA WAROPOKAJI WANA BABA YAO LOW BATI ANSATA DAMU MPAKA CHIAGULANYI PIA MWANAFUNZI WAKE. TUWAPUUZE NA TUCHAPE KAZI NA WANAJITAMBUA. TUSHIRIKIANE KWA MASLAHI YA PANDE ZOTE.

    YA TWIITA YABAKI TWITA MPAKA YAKIITWA.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad