Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema askari watakaoshindwa kuwabaini Wahamiaji haramu hususani maeneo ya mipakani wanapoingilia watawajibishwa ikiwemo kuondolewa kazini.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi mpya ya mafunzo ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Simbachawene amesema watawashughulikia askari wote wanaoingia katika mkoa ya mipakani ambapo wanaingia kwa mara ya kwanza wahamiaji hao.
Waziri Simbachawene amesema kitendo cha wahamiaji haramu kukamatwa maeneo mbalimbali ndani ya nchi, ambayo siyo mipakani ni kutokana na kuwepo na mawakala wanaofanikisha wahamiaji hao kuingia nchini.
“Wahamiaji haramu kama tukiwakata Morogoro na wakasema wameingia hapa Mkinga, sisi hatushughuliki na wale Morogoro, tutashughulika na waliopo Wilayani Mkinga na Tanga, tuwahoji wamepitajepitaje wahamiaji hawa haramu,” amesema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Pia tutawauliza polisi, ilikuaje musiwaone wahamiaji hawa haramu maana ‘barrier’ zote zenu, hawa hawatembei kwa miguu, walipanda gari, walipandia wapi gari, na kama wakituambia walipanda gari, hawa watu wote (Askari Polisi na Uhamiaji) wapo kwenye Wizara yangu, wote nitafagia.”
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI), Dkt. Anna Makakala, alisema mafunzo katika kambi huyo mpya, yanajumuisha jumla ya askari na maafisa wa uhamiaji 287, wanawake 81 na wanaume 206, ambapo mchanganuo wa kozi ya Mrakibu Msaidizi wapo 32, Mkaguzi Msaidizi wapo 112, kozi ya Sajini 42 na kozi ya Koplo wapo 101.