Hayo yameelezwa leo Jumamosi Januari 30, 2021 na kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Jerome Ngowi akibainisha kuwa Hussein akiwa njiani alijisikia vibaya na madereva wenzake walimpeleka hospitali ya Chimala na baada ya vipimo alikutwa na ugonjwa huo.
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya Peter Kigombola ambaye ni daktari aliyempokea, baada ya kugundua hali hiyo aliwaeleza anapaswa kutengwa na kulazwa.
Amesema kauli ya daktari huyo ilipingwa na madereva waliompeleka Hussein hospitali na walimchukua wakidai atakwenda kutibiwa katika hospitali iliyopo mamlaka ya mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe.
Amebainisha kuwa baada ya kutoka hospitali hiyo, Hussein aliendelea kuendesha gari huku akiyumba barabarani na aliyagonga magari mengine na wananchi walitoa taarifa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani kituo cha Inyara wilaya ya Mbeya.
Ngowi amesema baada ya kulizuia gari hilo walimwamuru Hussein kuteremka lakini alikaidi, askari wakalazimika kutumia nguvu kumshusha na kumpeleka kituo cha polisi.
“Kadri muda ulivyokwenda hali yake ilizidi kudhoofu
na hivyo askari waliokuwa zamu wakalazimika kumkimbiza kwenye kituo cha afya cha Igawilo kwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia,” amesema
Wakati polisi wakieleza hayo, mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa malori Tanzania, Abubakar Msangi ameomba kamati ya uchunguzi iliyoundwa na mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kukamilisha uchunguzi wake na kutoa taarifa sahihi za chanzo cha kifo cha Hussein.