Polisi Watano Watuhumiwa Uhalifu uwanja wa Ndege




Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameagiza maofisa watano wa polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuchukuliwa hatua za kinidhamu baada ya intelijensia yake kubaini wanajihusisha na matukio ya ukiukwaji wa maadili.


Simbachawene alisema amebaini maofisa hao wanajihusisha na mtandao wa kusafirisha mabinti kwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za uarabuni na kutumia nafasi zao kutapeli baadhi ya abiria.



“Nimewataja kwa majina na nimewakabidhi hawa viongozi na tutawachukulia hatua za kinidhamu kwa sababu tuna taarifa za kiintelijensia wanafanya vitendo hivyo ikiwamo kubabaisha abiria wakati wa kuondoka, wakiona abiria huyu ana uwezo wa kifedha wanafanya ubabaishaji,” alisema.



Simbachawene alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake katika vikosi mbalimbali vya Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam kwa lengo la kukagua na kutathmini utendaji kazi. Alisema Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu wanaochafua heshima ya jeshi hilo.



Hata hivyo, Kamanda wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini, Jeremia Shila aliyepokea agizo hilo aliliambia gazeti hili kuwa hatua itakayofuata kwa sasa ni uchunguzi ili kujiridhisha.



Alisema kwa sasa maofisa hiyo wataendelea kuwa kazini hadi ushahidi wa tuhuma hizo utakapokamilika.



“Ndio tumezipokea taarifa palepale, sasa ukipewa kitu (taarifa) inabidi unusenuse kidogo ili uweze kutekeleza agizo vizuri,” alisema Kamanda Shila huku akijivunia mchango wa teknolojia, mbwa na maofisa wake katika utendaji kazi uliokomesha matukio ya upitishaji wa dawa za kulevya.



Matukio mbalimbali ya maofisa hao ni pamoja na lile la Desemba 25, mwaka jana baada ya watu tisa wakiwamo askari polisi watatu kunaswa na kwa tuhuma za kumteka mwenyekiti wa Chama cha Wauza Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel na kumwomba rushwa ya Sh30 milioni.



Ziara hiyo ilianzia ofisi za makao makuu ya Idara ya Huduma kwa wakimbizi iliyoweka wazi kuwapo kwa wakimbizi 275,000 wanaoendelea kupata huduma mbalimbali nchini huku ikitarajia kufunga kambi moja kati ya tatu iliyopo Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma.



Pia Simbachawene alitembelea Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Kikosi cha Anga Tanzania alikoelezwa kuwapo kwa changamoto ya gharama za matengenezo ya ndege moja kati ya mbili, inayobeba abiria sita.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad