Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa Baraka zake kwa Taifa kutokana na kuliepushia janga la Corona ilihali ugonjwa huo ukiendelea kusababisha vifo vya maelfu ya watu katika nchi nyingine Duniani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia Vijana wadogo wa Kikatoliki mara baada ya Ibada ya Jumapili ya Pili iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Januari 17, 2020 alipoungana na waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato Mkoani Geita katika ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na Paroko wa parokia hiyo, Padre Henry Mulinganisa.
Akitoa salamu hizo amesisitiza kuwa kutokana na Tanzania kuepushwa na janga hilo wanatakiwa kuchapa kazi hasa kuzalisha mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula kwaajili ya kuzisaidia nchi ambazo zinashindwa kufanya uzalishaji.
“Sasa hivi mvua zinanyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, nawaombeni sana ndugu zangu Watanzania tulime mazao hasa ya chakula, tulime kwa wingi ili baadaye tuje kuwasaidia wenzetu ambao wanashindwa kulima kutokana na Corona”, amesema Dkt. Magufuli.