Dar es Salaam. Leo Jumanne Januari 19, 2021 Rais wa Tanzania, John Magufuli ameeleza sababu za kutomteua Profesa Makame Mbarawa kuwa waziri.
Kati ya mwaka 2015 hadi 2020, Profesa Mbarawa aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa waziri wa ujenzi na baadaye kuhamishiwa wizara ya maji.
Katika uteuzi wa baraza la mawaziri alioufanya mwishoni mwa mwaka 2020, Magufuli hakumteua Profesa Mbarawa.
Leo kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza sababu za kutomteua msomi huyo kuwa ni kushindwa kusimamia miradi ya maji.
“Katika miradi ya ovyo iliyofanyika ni pamoja na miradi ya maji na ndio maana sikumrudisha waziri wa maji kwa kuwa miradi ilikuwa na gharama kubwa na haikamiliki. Nina uhakika aliyepo sasa ataelewa hii changamoto.”
“Kipindi kilichobaki nitafanya kazi kwelikweli na wateule wangu wajipange kukimbia, ninataka yote niliyoahidi niyatimize atakayejipanga kunichelewesha atachelewa yeye,” amesema Rais Magufuli.