Sakata la Ozil Kutua Fenerbahce, Mbwana Samatta Kicheko tu, Ishu Ipo Hivi



HABARI njema kwa mashabiki wa Fenerbahce ya Uturuki na wafuasi wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ ni kutua kwenye klabu hiyo kwa supastaa wa Kijerumani, Mesut Ozil ambaye alifanya makubwa kwenye Ligi ya Ujerumani (Bundesliga), Hispania (LaLiga) na England (EPL).

Ipo imani kwa Watanzania Samatta anaweza kung’ara zaidi Ozil akitua Fenerbahce kutokana na uwezo alionao kiungo huyo katika kutengeneza nafasi za mwisho kote alipopita alikuwa mfalme wa asisti.


Tujikumbushe kidogo, wakati akiwa Ujerumani na klabu ya Werder Bremen msimu wa 2009/10, Ozil alitwaa tuzo ya kuwa mchezaji aliyetengeneza mabao mengi zaidi, 17, alimzidi Zvjezdan Misimovic wa VfL Wolfsburg kwa asisti mbili. Ndani ya msimu huo wa Ligi Kuu Ujeruman akawa kiungo bora wa msimu.

Ndani ya mwaka huo, 2010 alienda Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani alitwaa tena tuzo ya mtoaji asisti bora akitoa tatu. Ozil alionyesha ni balaa kwenye upigaji pasi za mwisho hata akiwa Hispania na Real Madrid na alitwa tuzo hiyo, 2010/11, 2011/12, 2012/13.

Hata alipokuwa na Arsenal huko England na alitwaa tuzo hiyo 2015/16. Sasa tuangalie mifumo mitatu ambayo inaweza kuwaunganisha Ozil na Samatta, je! anaweza kuendelea kile alichokuwa akikifanya Ujeruman, Hispania na England, atakuwa shujaa nyuma ya mabao ya Samatta? Twende sawa.


MFUMO WA 4-2-3-1

Katika michezo mitano ya hivi karibuni ya Fenerbahce, kocha wa hiyo, Erol Bulut ameonekana akitumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1. Samatta ndiye anayeonekana kuwa mshambuliaji wa mwisho na ameonyesha kuwa kwenye kiwango bora tangu atoke majeruhi kwani ametupia mabao mawili kwenye michezo miwili iliyopita.


Kwa mfumo huu, bila shaka langoni anaweza kuendelea kucheza Bayindir huku mabeki wakiwa Aziz Substituted, Novák, Tisserand na Sangaré, viungo wakabaji ni Luiz Gustavo na Tufan, kazi itakuwa kati ya viungo watatu wa nyuma ya Samatta kwenye mfumo huo wa 4-2-3-1.

Mmoja kati ya Pelkas, Valencia na Thiam anaweza kuanzia benchi ili kumpisha Ozil ambaye ana uwezo wa kucheza kama winga wa kulia au kushoto, pia anaweza kutumika kama namba 10 yani akacheza nyuma ya Samatta.


MFUMO WA 4-4-2

Kwa mfumo wa 4-4-2 ambao Fenerbahce walikuwa wakiutumia wakati Samatta akiwa majeruhi huku wakicheza Papiss Cissé na Mame Baba Thiam ambao wote ni raia wa Senegal, unatoa nafasi kwa Ozil kucheza akitokea pembeni au kuwa mmoja wa viungo wa kati lakini pia anaweza kucheza mbele na Samatta.


Ni eneo ambalo Ozil amekuwa akifanya vizuri zaidi hivyo itambidi kocha Bulut kutumia kiungo mmoja mkabaji ili kumpa nafasi fundi huyo wa Kijerumani.

ozil pic 1
Mara kadhaa Bulut amekuwa akipenda kuwatumia viungo wawili wakabaji ambao ni Gustavo, Tufan au Yandas au anaweza kuamua kubadilika kwa kutumia mfumo wa 4-5-1 akiwa na lengo la kuwa na viungo wawili wakabaji lakini mbele yao akicheza Ozil bila kuathiri nafasi ya mawinga pembeni huku mshambuliaji akisimama peke yake mbele na kusubiri mambo kutoka kwake.

MFUMO WA 4-3-3

Kabla ya Bulut kutumia mfumo wa 4-4-2 na 4-2-3-1 alikuwa muumini wa mfumo wa 4-3-3 ndio ambao alikuwa akiitumia mwanzoni kabisa mwa msimu kabla ya kubadili maamuzi na kuachana nao.

Pengine anaweza kurudi kwenye mfumo huo kutokana na uwepo wa Ozil kwenye kikosi chake, namna ambavyo anaweza kuingia kwenye mfumo huo ni kwa kutokea pembeni kati ya washambuliaji wa tatu wa mbele.

Namna nyingine ni kuwa kati ya viungo watatu nyuma ya watatu wa mbele kabisa kwenye ya ushambuliaji, wakati wenzake wawili wakiwa jukumu kubwa ya kukaba anaweza kupewa jukumu moja tu la kutengeneza nafasi za mabao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad