SIMBA ni raha tupu huku Kampeni ya WIDA ikijibu Uwanja wa Mkapa jijini Dar jana Jumanato baada ya Simba kupindua meza mbele ya FC Platinum kwa ushindi wa mabao 4-0 ambayo yameifanya isonge mbele hatua ya makundi ya mi-chuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbinu za Kocha Sven Vandenbroeck ambaye alianza na mshambuliaji mmoja, Chris Mugalu, zilijibu dakika ya 39 baada ya viungo Luis Miquissone na Clatous Chama kupeleka mashambulizi yaliyofanya Luis achezewe faulo ndani ya 18.
Mkongwe Erasto Nyoni hakuwa na huruma baada ya kumtungua kipa wa FC Platinum kwa penalti ya viwango na kuifanya Simba iende mapumziko ikiwa inaongoza kwa bao 1-0.
Bao hilo likaweka mzani sawa baada ya mechi ya kwanza kule Zimbabwe, FC Platinum kushinda 1-0.Kipindi cha pili FC Platinum walifunguka na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, pongezi kwa kipa Aishi Manula ambaye aliweza kuokoa michomo ya hatari iliyokuwa inatengenezwa na muuaji wao kwenye mchezo wa kwanza kule Zimbabwe, Perfect Chikwende.
Beki mkongwe, Shomari Kapombe aliandika bao la pili kwa mkwaju matata baada ya kipa kutema shuti la moto lililopigwa na kiungo Larry Bwalya nje ya 18, dakika ya 62.
Dakika ya 90+1, John Bocco ambaye aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Meddie Kagere ambaye aliumia muda mfupi baada ya kuingia akichukua nafasi ya Mugalu, alipachika bao la tatu kwa pasi ya Bwalya.Chama alimaliza msumari wa mwisho dakika ya 90+5 kwa penalti ambayo alifanyiwa madhambi yeye mwenyewe ndani ya 18. Simba ikajihakikishia ushindi wa mabao 4-0 na kusonga mbele kwa mabao 4-1.
Luis na Chama walikuwa nyota huku Said Ndemla ambaye alichukua mikoba ya Jonas mkude mambo yalikuwa mazito kwake kwa kuwa hakumaliza dakika 90.
Ushindi huo unaifanya Simba kucheza mechi tisa nyumbani katika michuano hiyo bila ya kupoteza. Matokeo ya mechi hizo ni; Simba 4-0 Mbabane, Simba 3-1 Nkana, Simba 3-0 JS Soura, Simba 1-0 Al Ahly, Simba 2-1 AS Vita, Simba 0-0 TP Mazembe, Simba 1-1 UD Songo, Simba 0-0 Platea United na Simba 4-0 FC Platinum.
Simba kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, ina uhakika wa kuomba kitita cha dola 550,000 ambazo ni sawa na Sh Bil 1.2 za Kitanzania ambapo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), huzitoa kwa timu zote zinazotinga hatua hiyo kwa msimu huu.