AMA kweli kabla hujafa hujaumbika! Kijana aliyefahamika kwa jina la Kagusa Kayola (27), mkazi wa Ubungo-Kibo jijini Dar, amejikuta kwenye mateso makali kiasi cha kupita kwenye bonde la mauti.
Kagusa anaugua ugonjwa wa sickle cell kwa kipindi kirefu, hali iliyomsababishia kuvimba miguu na tumbo kujaa maji.
Gazeti la IJUMAA limemtembelea Kagusa nyumbani kwao maeneo hayo na kuzungumza naye ambapo anasimulia mateso anayopitia na kukiona kifo chake mbeleni.
Kwa uchungu mkubwa, kijana huyo anasema kuwa alianza kuugua taratibu, lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya, kiasi cha kumfanya azimie mwezi mzima ambapo akizinduka anakuwa amepoteza kumbukumbu.
“Nimezaliwa na ugonjwa wa sickle cell. Nilipofikisha umri wa miaka mitano ndipo wazazi wangu walipogundua kuwa nina huu.
“Niliendelea kuishi nao hivyohivyo kwa muda mrefu na hakukuwa na matatizo yaliyojionesha.
“Ilipofika mwaka 2007 ndipo nikaanza kupata maumivu makali mno ya miguu, mikono na mgongo.
“Tulipokuwa tukienda hospitalini, haikufahamika tatizo ni nini hivyo nikawa ninatumia dawa za kutuliza maumivu.
“Niliendelea kuhudumiwa hivyo na wakati huohuo nikaendelea kusoma.
“Ilipofika mwaka 2008, mguu wa kulia ulianza kuvimba na nikawa ninahisi maumivu makali.
“Mwisho ikafikia hatua, nikawa ninashindwa kuvaa viatu, badala yake nikawa ninavaa sendozi.
“Nilipofika kidato cha tatu ndiyo maumivu yakazidi kiasi cha kupoteza fahamu darasani.
“Nilipokuwa ninazimia, nikipata fahamu ninaambiwa zimepita siku mbili labda au tatu, ikabidi nilazimike kuacha shule.
“Vipimo vikaendelea, nikapelekwa Muhimbili, Ocean Road wakasema hawaoni tatizo.
“Baadaye mguu wa kulia ukaanza kupata kidonda na kutoa usaa.
“Mwaka 2010 walikuja madaktari kutoka nchi za nje, nikatakiwa niende Muhimbili ili wanipime.
“Nilipopelekwa Muhimbili, nilifanyiwa vipimo, wakasema kwamba kidonda hakianzii kwa nje, kinaanzia ndani ndiyo maana mguu ukawa unavimba.
“Ilibidi nipasuliwe mguu ndipo ukaanza kutoka usaa mwingi.
“Madaktari walichukua vipimo vingine.
“Baada ya muda mrefu, wale madaktari wan je walituma majibu kwenye Hospitali ya Aga Khan.
“Majibu yalionesha kwamba bone marrow (uboho) inatakiwa ibadilishwe.
“Mwishoni mwa mwaka huohuo, nilianza kupata maumivu makali ya tumbo, baadaye likaanza kujaa maji, likawa kubwa na kila wakinipima, wakawa wanasema labda ni gesi.
“Kuna wakati madaktari walikuwa wakinipima hawaoni kitu, wakasema labda ni TB (kifua kikuu).
“Ilibidi wanipe dawa ambazo nilitumia miezi mitatu, ikafikia hatua nikashindwa hata kula. Niliunganishwa kwa daktari wa Kihindi ambaye alinifanyia Utra-Sound. Hapo majibu yalitoka kwamba tumboni mwangu kuna maji.
“Kilichofuata ni kutobolewa tumbo kisha kutolewa yale maji, lakini cha ajabu ukawa unatoka usaa.
“Nakumbuka kipindi hicho nilifanyiwa upasuaji kuanzia saa kumi jioni hadi saa sita usiku.
“Nilipozinduka, daktari aliniambia, nilipoteza maisha kwa dakika mbili ila Mungu akasaidia nikapata fahamu tena.
“Mwaka 2011 nilipata nafuu, nikawa vizuri na baba yangu alikuwa ameanza kuhangaikia taratibu za mimi kwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Mwaka 2012, baba yangu alikuwa amesafiri, aliporudi akaniambia ameshaweka mambo sawa hivyo bado mwezi mmoja tu, nitakwenda kutibiwa India, lakini kwa bahati mbaya, mwezi huo haukufika, baba tangu akawa amefariki dunia ghafla tu akiwa kibarazani.
“Tangu kipindi hicho, mambo yote yakabadilika na safari ya kwenda kutibiwa India ikaishia hapo.
“Baada ya miaka miwili, hali ikazidi kuwa mbaya, mguu wa kushoto nao ukaanza kusumbua.
“Mwaka 2016, nilianza kupata maumivu makali ya kichwa na miguu kiasi kwamba nilikuwa ninaona giza kisha nikapoteza fahamu. Nilipokuja kuzinduka, niliambiwa ulikuwa umepita mwezi mzima nikiwa kitandani bila fahamu, maana ilikuwa mwezi wa sita, nikaja kuamka mwezi wa saba mwishoni.
“Nilipozinduka kuinua mkono na kuongea, nikawa siwezi. Hata kumbukumbu nazo zikawa zimepotea, nikawa simkumbuki mtu yeyote hata jina langu pia. Zilipopita wiki tatu ndipo nikaanza kukumbuka baadhi ya vitu.
“Kipindi hicho daktari alisema kwamba kama ndugu zangu wana uwezo, basi wanipeleke India nikatibiwe, lakini mama akawa hana pesa. Ilibidi auze shamba letu maeneo ya Mbezi ya Kimaraea ndipo ikapatikana shilingi milioni 35 badala ya milioni 50 zilizokuwa zinatakiwa.
“Tulikwenda kwa daktari na kiasi hicho cha pesa, lakini tulishauriwa kwamba wakati ninapelekwa kutibiwa, basi inabidi tuombe serikalini.
“Kweli nilikwenda kutibiwa India kwa miezi mitatu, baadaye nikaruhusiwa, lakini mpaka ninafika Tanzania, nilikuwa siwezi kutembea ila angalau nilikuwa ninaweza kuinua mkono na kuongea.
“Ilipofika mwaka 2018 kuingia 2019 ndipo ugonjwa ukawa umezidi, muda wote nikawa ninasikia maumivu.
“Kuna dawa ya kupunguza maumivu nilitakiwa niwe ninakunywa kila siku, lakini ilikuwa ni bei ghali sana na nisipokunywa ninapata maumivu makali mno.
“Lakini kwa sasa hata hizo dawa sizinywi tena kwa sababu ya hali ya kiuchumi kuwa mbaya, imefikia hatua ninapoteza fahamu kila wakati kisha ninakuja kuzinduka baada ya siku au wiki kadhaa.
“Madaktari wameniambia ugonjwa wangu umezidi; yaani umefikia hatua ambayo ni mbaya mno, nisipopata msaada wa hali na mali ninakufa muda wowote nikiwa ninajiona.
“Naomba msaada wa haraka sana la sivyo itakuwa ngumu kwa hali yangu kuendelea kuwa sawa, naomba Watanzania wanisaidie, bado nina ndoto kubwa ambazo ninatamani kuzitimiza.
“Ninatamani hali yangu irudi kuwa nzuri kama zamani, naomba anayeweza kunisaidia matibabu.
“Madaktari wamenihakikishia kwamba nikifanyiwa hiyo ‘bone marrow’, hali yangu itakuwa nzuri, lakini pesa zinazohitajika siyo chini ya shilingi milioni 25,” alimalizia kusimulia Kagusa huku akimwaga machozi.