Dar es Salaam. Ofisa Programu wa Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC), Tito Magoti na mwenzake, Theodory Giyan mwanzoni mwa wiki hii walihukumiwa adhabu ya kulipa fidia ya Sh17,354,535 baada ya kupatikana na hatia kwa shtaka la kuongoza genge la uhalifu.
Magoti na Giyan ambaye ni mtaalam wa mifumo ya kompyuta, walitiwa hatiani Januari 5, mwaka huu na kuhukumiwa adhabu hiyo baada ya kukiri mashtaka.
Magoti na mwenzake awali walikuwa wakikabiliwa wakibiliwa na mashtaka matatu ya kushiriki au kuongoza genge la uhalfiu kwa kumiliki programu za kompyuta zilizotenegenezwa maalumu kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Mashtaka mengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 137 ya mwaka 2019 yalikuwa ni kumiliki programu za kompyuta kwa lengo la kutenda uhalifu na la tatu la kutakatisha fedha Sh17,354,535.
Hata hivyo, baada ya kufanya majadiliano na kuingia makubaliano DPP aliwafutia mashtaka mawili na kubakia na moja la kuongoza genge la uhalifu.
Kabla ya kupokea hati ya makubaliano hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega aliwauliza kama wameingia katika makubaliano hayo kwa hiyari yao wenyewe bila kushinikizwa na iwapo wanajua matokeo yake, nao wakakubali.
Hivyo, Wakili wa Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon aliwasomea shtaka hilo nao wakalikubali. Kisha walisomewa maelezo ya shtaka hilo ambayo ilikuwa mara ya kwanza kufahamika tangu wlipofikishwa mahakamani hapo.
Washtakiwa ni nani?
Kwa mujibu wa maelezo hayo yaliyosomwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, washtakiwa hao wanaelezwa ni akina nani, mahali wanapoishi na wanapofanyia kazi.
Wakati Magoti akitajwa ni mwajiriwa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kama afisa programu, mwenzake
Giyani ni mtaalam wa uendelezaji mifumo ya kompyuta ambaye hufanya kazi kama mshauri huru katika wa miradi inayohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kampuni ya ICT Prefixers Company Limited (IPF).
Magoti na Giyani wanatajwa kufahamiana tangu mwaka 2016 kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na walikuatana mara kwa kwanza mwaka 2018 katika bonanza lililoandaliwa na kundi liitwalo Tanzania On Twitter (TOT).
Walipokutana, wakili huyo aliieleza mahakama Magoti alimweleza mshtakiwa wa pili, Giyani kwamba kuna mpango wa kuanzisha kampeni kwa lengo la kusambaza taarifa alizosema za uwongo, upotoshaji na udanganyifu kwa umma kwa kisingizio cha haki za binadamu.
Alidai kuwa Magoti alieleza kuwa yeye ameandikishwa na mtu mmoja aliyeishi nje ya nchi akitumia namba za simu +447308329862 na +447572146716.
Vilevile anadaiwa kueleza kuwa mtu huyo amewaeleza kutakuwa na ujira mkubwa kwa yeyote atayekubali kushiriki katika mpango huo.
Kadushi anasema kwa maksudi ya kupata faida za kiuchumi, Magoti na Giyani walikula njama na wenzao wanaoishi ng’ambo kuunda ushirika wa uhalifu wa kupanga.
Katika kutekeleza njama hizo, walianzisha kundi katika mtandao kijamii wa WhatsApp kwa kutumia kompyuta walilokusudia lingetumiwa na wao peke yao pamoja na wenzao waliokula nao njama hizo.
Ili kuhakikisha kundi hilo lisiingiliwe na watu wengine isipokuwa wao tu, Kadushi anadai Magoti na Giyan walipewa line za simu zilizosajiliwa nchi za nje.
Magoti alipewa kadi ya simu yenye namba +31687908717, iliyosajiliwa nchini Uholanzi na Mshtakiwa wa pili alitumia kadi ya simu namba +31687252948 iliyosajiliwa pia nchini Uholanzi.
Mtu mwingine wa tatu anayedaiwa aliwaandikisha mshtakiwa hao alitumia kadi ya simu namba +31687637923, pia liyosajiliwa nchini Uholanzi.
Alidai kuwa washtakiwa hajawahi kusafiri kwenda Uholanzi wala kuzinunua wenyewe kadi walizokuwa wanatumia.
Baada ya kukamilisha kuunda mfumo huo wa utendaji uhalifu , Kadishi anadai walianza kuutumia kwa kutenda makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo uonevu wa kimtandao na kuchapisha taarifa za uwongo kunyume cha Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Makosa mengine wanayodaiwa kuyatenda ni kutoa kauli za chuki, kuibua hisia kali za kutokuridhika ambayo ni kinyume cha masharti yak Kanuni za Adhabu (Sura 16, Marejeo yam waka 2019).
Kwa mujibu wa maelezo hayo, ushahidi uliokusanywa umebaini kwamba kupitia mkakati wao wa uhalifu wa kupanga na katika kutenda makosa hayo yaliyotajwa hapo juu, walipokea malipo yasiyo halali ya Sh17,354,535 milioni kutoka katika mtandao wao wa kiuhalifu.
Washtakiwa walijipatia fedha hizo wakati wakijua kuwa pesa hizo ni mazao ya kosa tangulizi la utakatishaji fedha haramu, yaani kushiriki katika genge la uhalifu wa kupanga.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mtega aliwauliza kama maelezo hayo ni sahihi nao wakakubali ndipo akawatia hatiani na kuwahukumu adhabu hiyo ya kulipa fidia hiyo na kuwaachia huru kwa sharti la kutokutenda kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja
Source: Mwananchi