WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ametoa taarifa mpya juu ya kinachoendelea kufuatia kufungiwa Wasafi TV kwa miezi sita.
Bashungwa ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria za TCRA, wameifungia Wasafi TV, lakini wizara inaendelea kufanya jitihada za kupata mwelekeo utakaolinda ajira zilizozalishwa na Wasafi TV na uwekezaji uliofanyika bila kuvunja sheria za nchi.
Waziri Bashungwa aliyasema hayo Januari juzi, jijini Dar alipokuwa akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye kikao alichofanya na waandishi wa habari.“Wasafi TV kwa mujibu wa sheria za TCRA walifungiwa kwa maana sheria na kanuni zinasema ukikosa nini kifanyike, lakini sisi Wizara ya Habari kwenye jukumu la ulezi na kulitazama kwa mapana, inagusa ajira za vijana ambao wameajiliwa na TV hii, linagusa masuala ya uwekezaji.“
Tumewasiliana na TCRA kwa upande wao lazima tuendelee kushirikiana kuhakisha mila, desturi na sheria zinasimamiwa na kunakuwa na nidhamu katika tasnia ya habari.
“‘Lakini kwa malengo mengine ambayo nimeyataja ukiangalia upande wa ajira, uwekezaji na kwa malengo mapana ya kukuza tasnia ya sanaa sheria pia imeeleza ni nini kifanyike pale aliyewa adhabu ataona inafaa kuomba rufaa, sasa kupitia rufaa hiyo na kwa mapana niliyoyazungumza ya kukuza na kuhakikisha tasnia ya sanaa zinasimamia sheria, lakini wakati huo huo kupitia Wizara yangu tunaweka mazingira wezeshi na hili jambo litapatiwa mwafaka muda si mrefu,” alisema.