Watumishi 23 wa Kitengo cha Famasia cha Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa tuhuma za kuandika taarifa za uongo katika mfumo wa utunzaji taarifa za kumbukumbu za utoaji dawa na vifaa tiba, na kusababisha upotevu wa dawa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2.
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari, 13, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa watumishi hao wanadaiwa kufanya udanganyifu huo kati ya mwaka 2018 hadi 2020.
Akielezea namna ubadhirifu huo ulivyofanyika, Brigedia Mbungo amesema watuhumiwa hao walikuwa wanaandika taarifa za uongo katika mfumo huo, kwa kuweka idadi kubwa ya vifaa vilivyotolewa tofauti na idadi halisi iliyotolewa kwa wateja na madaktari.
"TAKUKURU kwa kushirikiana na MOI imedhibiti uchepushaji na ubadhirifu wa madawa ya zaidi ya Tsh Bil. 1.2, ambazo zilihujumiwa kwa manufaa binafsi na watumishi wa kitengo cha famasia katika taasisi hiyo"amesema Brigedia Mbungo.
Brigedia Mbungo ameongeza kuwa, "Ubadhirifu huu umebainika kutokana na uwepo wa tofauti kati ya taarifa za dawa zilizoingizwa na wafamasia na zile zilizoandikwa na madaktari ikilinganishwa na fomu za wagonjwa zilizotoa maelekezo ya aina ya dawa".
Brigedia Mbungo amesema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na kwamba mahojiano yakikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.