Tatizo ni Diamond mwenyewe, si Nyange wala mama Dangote



Diamond Platnumz ana umri wa miaka 31 kwa sasa. Ni mtu mzima. Ni baba wa watoto wanne wanaotambulika.


Wawili kutoka kwa cheupe wa Uganda, Zari The Boss Lady; supermodel Hamisa Mobetto anaye mmoja, kisha Tanasha Donna kutoka kwa Kenyatta.


Akiwa na umri huo, dunia inapokea ‘surprise’ kutoka kwa mama yake, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’ kuwa yule mzee aliyefahamika kwa miaka na miaka ndiye baba mzazi wa Diamond, kumbe siye. Ni mwingine tena jina jipya.


Abdul Juma wa Kariakoo, ndiye baba mzazi aliyefahamika wa Diamond. Naye Diamond akajitambulisha kwa sauti na nyaraka mbalimbali kuwa ni Nassibu Abdul Juma.


Ulipoingia mwaka 2021, Mama Dangote akasema “taarifa ya awali haikuwa sahihi”. Watu wakabaki midomo wazi; taarifa sahihi ni ipi? Jina “Salum Idd Nyange” likatajwa.


Kwa mujibu wa mama Dangote, huyo Salum wa Nyange ndiye damu ya Diamond. Kwamba Abdu wa Kariakoo alisingiziwa tu. Ni ya ulimwengu kwa walimwengu, Sheikh! Ingia ndani ya sanduku la ubongo wa Abdu.


Unaweza kupata tafsiri mbili; mosi, maumivu baada ya kuaibishwa. Siku zote alijitambulisha kuwa ni baba wa Diamond. Tena, Diamond si anajiita Simba? Abdul akajiita Big Lion. Kwani hujui kuwa Simba kwa Kiingereza ni lion? Abdu a.k.a Anko Dudu la Yuyu, akajitambulisha ndiye simba mkubwa!


Pili, kwa miaka mingi kumekuwa na mgogoro usio na majibu. Diamond haivi na baba yake. Wakati Mama Dangote akionekana kufaidi matunda ya mafanikio ya kijana wake, Abdu anateseka kwenye lindi la umaskini.


Shida nini? Mengi yamekuwa yakisemwa. Ooh, Abdu alimtelekeza Diamond akiwa mtoto, eti ndio alikuwa anapokea malipo yake. Abdu sasa anawaza: “Kumbe haya yote ni kwa sababu sio mtoto wangu!” Abdu naye mara kwa mara amekuwa akitoa utetezi, kwamba hakumtekeleza mwanaye, isipokuwa aligombana na mama Dangote kipindi Diamond akiwa kidato cha kwanza.


Kisha, mama Dangote akabaki na mwanaye.



Kuyaongea ya Diamond na Abdu ni kusababisha msongamano kwenye ubongo.


Yameshazungumzwa mengi. Tupo kona nyingine. Ni baada ya mama Dangote kusema Diamond si wa Abdu bali ni damu ya Salum wa Nyange.


Kwa kauli hiyo ya mama Dangote, yupo mwanafunzi wa darasa la sita anajiuliza leo; je, Diamond alishaambiwa kitambo kuwa Abdu sio baba yake mzazi ndio maana huwa hamjali? Mama Dangote kasema mchambuzi wa soka Wasafi FM, Ricardo Momo, ni baba mmoja na Diamond.


Inafahamika kuwa kwa miaka michache sasa, Ricardo yupo karibu sana na Diamond. Yupo mwanafunzi aliyefaulu mtihani wa darasa la nne hivi karibuni hataki kabisa kuamini somo kwamba Diamond na Ricardo walianza kuwa marafiki halafu ndipo ikagundulika ni mtu wa ndugu yake.


Huyu mwanafunzi aliyeingia darasa la tano Januari hii, ananishawishi kuamini kuwa hakuna bahati mbaya katika suala la Diamond, Ricardo na Mama Dangote.


Kosa la nani? Wengi wanamlaumu Mama Dangote. Kwamba amezingua ‘big time’ kusema Diamond ni damu ya Salum Nyange. Mimi simlaumu maana sidhani kama anastahili kulaumiwa leo. Kwani Diamond alizaliwa lini?


Mimba yake iliingia tumboni siku gani? Usisahau msemo kuwa ajuaye baba halisi wa mtoto ni mama. Rejea miaka 31 nyuma, ifikie Oktoba 2, 1989. Hiyo ndio siku ambayo Diamond alizaliwa. Anzia hiyo ‘birthday’ ya Diamond, halafu hesabu miezi tisa nyuma. Ni hapo utaweza kubaini siku kosa la mama Dangote lilipofanyika.


Alipogonganisha magari. Akanasa ujauzito. Ikawa siri. Abdu akaambiwa ni mzigo wake, naye akaupokea.


Kimahesabu, kosa la mama Dangote ni la miaka 32 iliyopita.


Kama ni lawama au adhabu, alipaswa kulaumiwa au kuadhibiwa kipindi hicho. Akaficha, ama alimficha Abdu au aliwazuga walimwengu. Jiulize, kwa nini ameamua kuyasema haya leo? Urahisi ni upi? Ukijiuliza maswali hayo vizuri ndipo utajua tatizo halisi lilipo. Ni Diamond Platnumz. Ameshakuwa mtu mzima, ni baba, maarufu, anayo heshima ambayo anapaswa kuilinda.


Hata hivyo, kwake mama yake imekuwa rahisi kumbadilishia baba. Mtoto yupo kimya. Unadhani kesi ya Diamond haifanani na wengi kwenye jamii? Wapo akina mama wanakufa na siri za baba halisi wa watoto wao.


Sababu ni hofu. Unaanzaje kumwambia mtoto anayejitambua kuwa “baba yako sio Abdu ni Salum wa Nyange”. Inawezekana vipi?


Kingine, akina mama wengi hufanya makosa kwa kunasa mimba nje ya ‘line’. Kwa kumheshimu mtoto wake, anamtambulisha mwanaye kwenye ‘line’, inabaki hivyo mpaka kifo.


Watoto wengi ambao wamelelewa na baba wasio wao, wamekufa, wanakufa na watakufa pasipo kujua ukweli kuwa baba zao wazazi sio waliowalea.


Mama anayemheshimu mwanaye, hawezi kumyumbisha, leo anamwambia baba yake ni Abdu, kesho Salum wa Nyange. Hapo unakuwa hujui kama kuna siku atamtaja Anko Shamte au yeyote yule atakayependa kumtunuku.


Ukifika hapo jiulize; Diamond amejiweka kwenye kundi gani? Hajitambui ndio maana mama yake anampelekapeleka? Na kwa nini anakubali kudhalilishwa ukubwani? Mpaka anafikisha umri wa 31 bado anatajiwa baba?


Diamond angekuwa amewahi kumuonesha mama yake kuwa hapendi ujinga, Mama Dangote asingethubutu kumleta Salum wa Nyange kwenye uso wa umma na kumtambulisha ndiye baba halali wa Diamond.


Angeogopa. Na angethubutu basi leo pangechimbika kati ya mtoto na mama. Rudia tena swali, kama Diamond alipokuwa na umri wa miaka 10 mpaka 15, hakuambiwa ukweli kuwa baba yake sio Abdu bali Salum wa Nyange, kwa nini aambiwe leo? Hutakosea ukisema Diamond alipokuwa na umri wa miaka 10, aliheshimiwa na mama yake kuliko sasa. Mama Dangote ameona Diamond wa sasa anaweza kuambiwa chochote na asifanye lolote kuliko yule wa miaka 16 iliyopita.




Luqman Maloto

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad