Uingereza itafungua leo vituo saba vya kutoa chanjo ili kuongeza kasi ya kuwachanja watu dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.
Waziri wa Afya nchini humo Matt Hancock amesema kwa sasa nchi yake inatoa chanjo kwa takriban watu 200,000 kila siku lakini inataka kuongeza idadi hiyo hadi watu milioni 2 kila wiki. Uingereza ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.
Duniani kote, maambukizi ya virusi vya corona yamepindukia watu milioni 90 na takriban watu milioni mbili wamefariki.
Nchi kadhaa pia zimeendelea kurekodi aina mpya ya kirusi cha corona kinachosambaa kwa kasi. Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameiita hatua ya watu kukwepa kupata chanjo ya COVID-19 kuwa mauaji ya kujitakia akisema wale wanaokataa chanjo hiyo wanacheza na afya zao na pia maisha ya watu wengine.