Dar es Salaam. Siku moja baada ya agizo la Rais John Magufuli kutaka ujenzi wa haraka wa madarasa ufanyike katika shule ya msingi King’ongo, viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wamepiga kambi kuhakikisha wanatekeleza amri hiyo.
Mapema jana gazeti la Mwananchi lilifika shuleni hapo na kumkuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Beatrice Dominic akisimamia shughuli za ujenzi huku akiambatana na viongozi wengine akiwemo Ofisa Elimu ya Msingi pamoja na Meya Jafari Nyaigesha aliyekuja baadaye.
“Hatujalala tangu jana tumeanza kufanya kazi hii, tumelipokea kama agizo na tunalifanyia kazi na imekuwa funzo kwetu,” alisema Beatrice.
Viongozi hao pia walikuwa hapo ikiwa ni muda mfupi tangu walipotembelea eneo hilo juzi wakiambatana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge
Wote hawa walifika shuleni hapo na kuanza kusimamia ujenzi wa madarasa nane ambayo mpaka gazeti hili linaondoka tayari kazi ya kumwaga zege ilikuwa imeanza kwa kasi.
Wakati hekaheka zikiendelea watendaji waliendelea kuongezeka shuleni hapo huku barabara zake nazo zikifanyiwa ukarabati kuanzia jana.
Ujenzi huo ni matokeo kusambaa kwa video iliyokuwa ikionyesha wanafunzi hao wakikaa chini ya miti wakati wakisoma huku mwalimu akitumia daftari kama ubao.
Pia katika video hiyo, uhaba wa madarasa na madawati ulizungumziwa huku ukionyesha baadhi ya wanafunzi waliopo madarasani wakitumia viroba kutandika chini ili wajifunze jambo ambalo lilionekana kumuudhi Rais na haraka akatoa maagizo ya changamoto hizo kutatuliwa haraka.
“Kuna shule ipo Dar es Salaam, Ubungo bado wanafunzi wanakaa chini, madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika, mkuu wa wilaya yupo, mkuu wa mkoa yupo, mkurugenzi yupo na mbunge wa Ubungo yupo tena yupo hapa ni profesa.
“Namshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao, viongozi wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa, hayo mambo ndio napenda kuyajua, nazungumza nikiwa Kagera nikifika Dar es Salaam niyakute madarasa yamekamilika na wanafunzi hawakai chini, nitakwenda kuitembelea, kama wanasikia `message sent’ (ujumbe umefika),” alisema Magufuli alipokuwa akizungumza juzi na wananchi katika Shule ya Sekondari ya Ihungo, ambayo imekarabatiwa.
Ujenzi huo wa madarasa nane ulioanza mara moja utaifanya shule hiyo yenye wanafunzi 2,505 hadi jana kwa mujibu wa walimu kuwa na madarasa 17 na moja litatumiwa kama ofisi ya walimu.
Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Elimu msingi wilaya ya Ubungo, Abdul Buheti alisema shule hiyo imeelemewa na wanafunzi ikiwa ni baada ya sera ya elimu bure ambapo wazazi walijitokeza kwa wingi kupeleka watoto wao.
“Tunatarajia ndani ya wiki mbili au chini ya hapo madarasa haya yawe yamekamilika na kutumika kwa sababu yatakuwa na madawati,” alisema.
Alisema ujenzi wa madarasa hayo utagharimu Sh20 milioni kila moja.
“Na niweke sawa, hakuna wanafunzi waliokuwa wanakaa chini, ila hao mliowaona katika video ni wanafunzi wanaoingia kwa awamu sasa kama wanaingia mchana baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatoa nyumbani mapema hivyo, walimu ndo wanawakusanya na kuwaweka hapo,” alifafanua ofisa huyo.
Wakati Ofisa elimu akiyasema hayo, Maulid Shikila ambaye ni mzazi alisema wanafunzi shuleni hapo kusomea nje ni suala la kawaida.
“Tunashukuru kwa madarasa waliyojenga lakini hayatoshi, maana hii ya wao kukaa chini ni suala ambalo lilikuwapo muda mrefu,” alisema Shikila.
Hiyo ni kwa sababu chumba kimoja cha darasa kwa mujibu wa takwimu kitatumiwa na zaidi ya wanafunzi 156 ikiwa ni mara tatu zaidi ya uwiano wa serikali wa chumba kimoja cha darasa kutumiwa na wanafunzi 45.
“Na kama wazazi tayari tulikuwa tumeanza mchakato wa kujenga madarasa mawili ikiwa ni makubaliano ya kikao tulichokifanya siku chache nyuma. Hata hizo tofali mnazoona hapo na kokoto ni mchango ya wazazi,” aliongeza.
Alisema kutokana na hali hiyo wanafunzi wanaofanya mitihani ya
Pamoja na kupunguzwa kwa changamoto ya madarasa pia shule hiyo ina uhaba wa vyoo
Licha ya kuwa na wanafunzi 2505 hadi jana, shule hiyo ina matundu 12 ya vyoo ambavyo vitano ni kwa ajili ya wavulana na vitano ni kwa ajili ya wasichana na vingine viwili vikiwa kwa ajili ya walimu
“Hatuna tatizo la vyoo hapa, kwa sasa tumejikita kutatua changamoto ya madarasa kwanza,” alieleza ofisa wakati akizungumza kuwepo malalamiko ya tatizo la vyoo