Dar/Mpwapwa. Mbunge mstaafu na mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (Kadco), Gregory Teu amefariki dunia jana baada ya kujisikia vibaya wakati akiwa kikaoni jijini Arusha.
Kifo cha Teu kimetokea, huku kukiwa na mfululizo wa vifo vya watu maarufu nchini ndani ya Januari katika nyanja za siasa, sanaa, sekta ya umma na viongozi wa dini.
Teu aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Mpwapwa (CCM) kati ya mwaka 2010 hadi 2015 na kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa naibu Waziri wa Fedha na baadaye naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.
Pia Teu aliwahi kuwa Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Mpwapwa katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Kadco Oktoba 17, 2017 baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, Balozi Hassan Kibelloh.
Akizungumza jana wilayani Mpwapwa, msemaji wa ukoo wa Teu, Stanley Mbijili alisema mwenyekiti huyo alikuwa kwenye kikao cha Bodi ya Kadco jijini Arusha ambapo alijisikia vibaya na kupelekwa hospitali juzi.
Mbijili alisema Teu alifariki dunia saa 9:00 alfajiri usiku wa kuamkia jana wakati akiendelea na matibabu katika hospitali ambayo haijafahamika.
“Tunajua kuwa marehemu (Teu) alikwenda Arusha kwenye kikao cha bodi kwa sababu yeye alikuwa ni mwenyekiti wa bodi hiyo ila hatujajua alikufa katika hospitali gani,” alisema.
Alisema utaratibu wa kusafirisha mwili wake utafanyika kesho Januari 27 kutoka Arusha kwenda Mpwapwa na kwamba mazishi yatafanyika Jumatano (Januari 28) katika makaburi yaliyopo katika viwanja vya Kanisa la Watakatifu Wote Vighawe.
Msemaji huyo alisema Teu alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na sukari mara kwa mara.
Mbali na kifo hiyo, Januari pia imeshuhudia vifo vya watu maarufu wakiwemo wasanii na wanasiasa.
Juzi, Januari 24 aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya usafiri wa mwendokasi (Udart), David Mgwassa alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Juhudi za kumpata msemaji wa familia ya Mgwassa hazikufanikiwa jana, lakini taarifa kutoka kwa ndugu wa familia hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini zilisema, mazishi ya Mgwassa yanamsubiri mtoto wake anayeishi Canada na anatarajia kuzikwa jijini Dar es Salaam.
Januari 17 mwaka huu, jumuiya ya wasanii ndani ya nje ya nchi ilimpoteza mwanamuziki Ilunga Khalifa maarufu kama `Cpwaa’.
Msanii huyo wa Bongofleva alikutwa na umauti wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa baba yake mzazi msanii huyo, Khalfani Juma, mtoto wake alikuwa anasumbuliwa na homa ya mapafu, ugonjwa ambao ulimsababishia kifo.
Siku tatu baadaye Januari 20, Kamishna wa Jeshi la Magereza, Jenerali Suleiman Mzee alitoa taarifa za kifo cha Naibu Kamishina wa jeshi hilo, Julius Sang’uti.
Sang’uti alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma.
Siku hiyo hiyo ya Januari 20 Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Manyara, Martha Umbulla alifariki dunia katika Hospitali ya HCG Mumbai, India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa ya kifo cha mbunge huyo ilitolewa Januari 21 na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Martha Umbulla. Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wabunge na wananchi wa Mkoa wa Manyara. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Januari 21, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya siasa, Prudence Karugendo alifariki dunia. Karugendo alikuwa mwandishi mahiri wa makala za siasa.
Wakati bado machungu ya vifo hivyo hayajaisha, usiku wa kuamkia Januari 22, Watanzania walipata tena simanzi kufuatia taarifa za kifo cha aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga.
Maganga alifariki dunia katika Hospitali ya Jeshi ya Mirambo Manispaa ya Tabora alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Phillemon Sengati, kiongozi huyo mstaafu alifikwa na mauti muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Alisema kulingana na maelezo ya watu wa karibu, marehemu alikuwa akijisikia maumivu ya mwili kwa wiki moja iliyopita ambapo alikuwa akitumia dawa lakini hali ilizidi kuwa mbaya usiku wa kuamkia Januari 22 na kupelekwa hospitalini ambako mauti yalimfika.
Januari 22 pia alifariki Padri wa Jimbo Katoliki Bukoba, Ireneus Mbahulira. Padri Mbahulira alifariki katika hospitali ya Mugana wilaya ya Misenyi alipokuwa amelazwa takribani wiki moja akipatiwa matibabu.
Askofu Msaidizi wa jimbo la Bukoba Methodius Kilaini alisema kifo hicho kimetokewa ikiwa ni wiki moja baada ya padri huyo kulazwa hospitalini hapo.
Alisema baada ya kulazwa hospitalini hapo aliwekewa dripu za maji ya kumwongezea nguvu mwilini na kuna wakati aliwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua.
Mwananchi
Watanzania, Tuenddelee kumuomba Mungu na tuanze zoezi la NYUNGU SEASON 4 Ya
ReplyDeletenguvu Nchi nzima.
Mwenyezi mungu aendelee kutulinda na kutupa Afya.