Viongozi Kilimanjaro wakanusha mwanafunzi kuugua Corona, shule yaomba radhi

 


Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kufungwa kwa shule ya International School Moshi (ISM) kwa madai ya mwanafunzi mmoja kukutwa na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.


Wakati uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro ukikanusha habari hizo, mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Marsden mbele ya wanahabari leo Alhamisi Januari 21, 2021 ameomba radhi kutokana na kusambaa kwa taarifa kuwa shule imefungwa na kusimamisha masomo, akisema ukweli ni kwamba masomo yanaendelea kama kawaida.


Madai hayo chanzo chake ni taarifa za ndani kutoka katika shule hiyo zilizowekwa katika tovuti yake Januari 19,2021 akitaarifu juu ya kuwepo kwa mwanafunzi aliyethibitika kuwa na Covid-19.


Kwa mujibu wa maagizo ya Serikali, ni viongozi wanne tu wanaotoa taarifa za Corona ambao ni rais, waziri mkuu, waziri mwenye dhamana ya afya na msemaji mkuu wa Serikali.


Leo katika maelezo yake,Mghwira ameieleza Mwananchi Digital akiwa mkoani Tanga kwamba kiini cha mtafaruku ni watoto wawili wa familia moja ambao shule iliwahisi kuwa na Covid-19.


Amesema kutokana na hali hiyo na baada ya taarifa kusambaa katika mitandao wa kijamii, alimtuma msaidizi  wake pamoja na ofisa elimu wa mkoa ili waende katika shule hiyo kufahamu nini kilitokea.


Mkuu wa wilaya ya Moshi, Rajabu Kundya na meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu kwa nyakati tofauti wamekanusha  uwepo wa mwanafunzi aliyeathirika na virusi hivyo vya Corona.


Kabla ya kuzungumza na wanahabari, mkuu huyo wa wilaya na maofisa wengine wa Serikali walikuwa na vikao vya faragha na uongozi wa shule hiyo, wakifuatilia taarifa hiyo ambayo iliibua mtafaruku nchini.


“Kwanza shule haikufungwa. Wanafunzi wanaendelea na masomo na vikundi vya mjadala kama kawaida. Kwenye chakula wamekaa pamoja na hakuna tuliyemuona amevaa barakoa. Kwa hiyo, hiyo peke yake ni ishara kwamba taarifa ile ilipotoshwa,” amesisitiza mkuu huyo wa wilaya na kusema shule hiyo iko makini kwa vile inapokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani.


“Shule hii ni shule inayopokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani na tatizo hili liko katika nchi nyingine nyingi zikiwemo hata jirani zetu hapa, wamekuwa makini pale ambapo mtoto anaoonekana anazo dalili.”


“Akionekana na dalili zinazoendana na tatizo hilo Covid-19, basi haraka zinachukuliwa hatua za tahadhari ili kuzuia kwa dalili hizo asiwaambukize wengine,” alisema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa,” amesema.


Akifafanua zaidi amesema, “ndio sababu hata mtindo wa ufundishaji ukabadilika lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba kama anapatikana mtu mwenye tatizo hilo au jingine linaloweza kuambukiza anadhibitiwa ili tatizo hilo lisienee kwa wengine.”


“Ninachopenda kuwahakikishia watanzania ni kwamba shule haikufungwa iko salama. Wilaya ya Moshi iko salama, mkoa wa Kilimanjaro uko salama na Tanzania iko salama bila Covid19.”


Kilichoandikwa kwenye tovuti


Kwa mujibu wa tovuti hiyo, kampasi ya Moshi na Arusha zina jumla ya wanafunzi 600 kutoka mataifa 80 duniani huku kampasi ya Moshi pekee iliyoanzishwa miaka 51 iliyopita ikiwa na  wanafunzi 300.


“Mwanafunzi wa darasa la M4 kampasi ya Moshi alithibitika kuwa na maambukizi ya Covid-19 Januari 18 (2021). Januari 19 mwanafunzi mwingine alionyesha dalili za Covid-19 ingawa alikuwa hajapimwa.”


“Kwa sababu hiyo, kampasi ya Moshi imesitisha kwa muda ufundishaji wa ana kwa ana na kuhamishia mafunzo yote kwa njia ya mtandao mpaka Februari 1,2021. Taarifa kamili iko kwenye barua pepe ya mkurugenzi”


Taarifa hiyo ilifuatiwa na taarifa ya mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Marsden katika tovuti hiyo akisema kutokana na tatizo hilo la Covid 19, kampasi ya Moshi ya ISM itakuwa katika karantini hadi Februari mosi,2021.


“Wakati inabaki kuwa tuna mwanafunzi mmoja tu mwenye Covid-19, sasa tuna mwanafunzi wa pili ambaye anaonyesha dalili ambazo zinaweza kuhusishwa na virusi vya corona,” amesema Anna katika taarifa hiyo.


Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa wanafunzi wa kutwa watasoma kwa njia ya mtandao kutokea nyumbani na wale wa bweni watabaki katika mabweni yao na kwamba walimu wote watafanyia kazi wakitokea nyumbani.


 “Kwa hiyo wageni waendelee kuja wakijua wanakuja mahali salama. Ningependa sana mitandao ya kijamii izingatie utaratibu wa nani ni msemaji wa tatizo gani ili wapate taarifa kutoka chanzo sahihi,” amesema.


Kundya alisema hiyo itaisaidia mitandao hiyo kutoa kutoa taarifa sahihi akieleza kuwa taarifa hizo za ISM zimeleta taharuki kubwa Moshi mjini lakini walipofuatilia wamekuta kilichoandikwa na hali halisi havifanani

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad