Chama cha walimu nchini Kenya (KUPPET) kinaitaka serikali kutoa mafunzo ya usalama kwa walimu na kuwapa silaha wale wanaopelekwa kufundisha kwenye maeneo yaliyo ya hatari.
Kaimu Katibu Mkuu wa KUPPET Moses Nthurima amesema kuwapa walimu silaha si kuwa tu kutawaogopesha watu wanaowashambulia lakini pia kutawapa walimu hali ya kujiamini kufanya kazi katika mazingira ya hatari.
“Tunarudia ombi hilikwamba katika hali ya ukosefu wa usalama, lazima walimu wafundishwe na kupatiwa bunduki.''
''Huwezi kumkabili mtu mwenye bunduki kwa kutumia chaki. Tunapompeleka mwalimu katika maeneo ambayo usalama ni mbovu mwalimu ataishi kwa hofu kila wakati. Lakini ikiwa bunduki inaning'inia mgongoni hata majambazi watajua kuwa mwalimu ni eneo lisilofaa na watachukua sekunde kufikiri kabla ya kufanya makosa, "Alisema Bw. Nthurima.
Ombi hilo limekuja baada ya kutokea matukio ya kuuawa kwa walimu na watu wenye silaha katika maeneo ya Kaskazini-Mashariki na Pwani ya Kenya.