Muungano wa walinda usalama katika eneo la Dafur nchini Sudan, kutoka umoja wa Afrika na umoja wa mataifa – UNAMID, unamaliza mda wake eneo hilo hii leo alhamisi, baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 13. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, muungano huo wa kijeshi umesema kwamba serikali ya Sudan itachukua jukumu la kuhakikisha kwamba eneo hilo lina usalama wa kutosha. Wiki iliyopita, baraza la usalama lenye wanachama 15, lilikubaliana kwa Pamoja kuondoa wanajeshi hao katika eneo hilo kuanzia leo, kufikia June tarehe 30 mwaka ujao 2021. Wanajeshi wa umoja wa mataifa na umoja wa Afrika, wamekuwa Dafur tangu mwaka 2007, katika juhudi za kumaliza mapigano mabaya yaliyotokea eneo hilo la magharibi mwaka 2003 kati ya wanajeshi wa serikali na makundi ya waasi. Kulingana na umoja wa mataifa, wanajeshi 4,000, washauri wa polisi 480, polisi 1,631, wafanyakazi wa kiraia wa kimataifa 483 na wafanyakazi wa kiraia wa Sudan 945 wanafanya kazi ya usalama eneo la Dafur, Sudan. Watu 300,000 wameuawa na wengine milioni 2.5 kuachwa bila makao kufuatia vita vya Darfur.