Wapinzani wa Rais wa Marekani Donald Trump katika mabunge yote mawili wametoa wito wa rais huyo kuondolewa madarakani baada ya wafuasi wake waliokuwa wakifanya vurugu kuvamia bunge.
Seneta wa Democratic Chuck Schumer amesea Bwana Trump anastahili kuondolewa mara moja. Na ikiwa sio hivyo, Spika wa bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema anaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Kuondolewa kwa rais huyo kupitiamuswada wa kutokuwa na imani naye, kutahitaji kuungwa mkono na wabunge wa Republican ambao kufikia sasa ni wachache tu wanaoonekana kutofautiana naye.
Katika hotuba iliotumwa kwa njia ya video, Bwana Trump alisema amejitolea kukabidhi mamlaka kwa amani.
Rais huyo alisema utawala mpya utaapishwa Januari 20 na kutoa wito wa "maridhiano".
Pia alisema, "hasira imesababishwa na vurugu, uasi wa sheria na ghasia" zilizotokea Jumatano na kwamba "hasira lazima zitulizwe". Video hiyo ilishirikishwa kwenye akaunti yake ya Twitter, ambayo iliwezeshwa tena kutumika kuanzia Alhamisi baada ya kufungwa kwa muda kwasababu ya tukio la uvamizi wa bunge.
Watu wanne walifariki dunia wakati wa uvamizi huo huku wengine 68 wakiwa wamejeruhiwa.
Sasa hivi maafisa wa polisi wameanza kuchunguzwa jinsi walivyoshughulikia maandamano hayo na kukosolewa kwa kushindwa kusitisha waandamanaji kuvunja sheria na kuingia bungeni.
Maafisa waliokuwa walinda usalama katika Bunge la Wawakilishi ikiwa ni pamoja na muongozaji shughuli za bunge wamejiuzulu.
Taarifa zinasema mkuu wa polisi bungeni Steven Sund pia naye anajiuzulu kuanzia Januari 16 kufuatia wito uliotolewa na Bi. Pelosi.
Bwana Schumer upande wake anataka wenzake wa bunge la Seneti kufutwa kazi.
Waziri wa usafirishaji Elaine Chao ndio wa hivi karibuni kujiuzulu katika utawala wa Trump kwasababu ya maandano hayo.
Maafisa kadhaa wa ngazi ya chini pia wamejiuzulu.
Rais mteule Joe Biden amesema: "Hivi unasema kama hapo jana ingekuwa ni maandamano ya kundi la Black Lives Matter hatua zilizochukuliwa dhidi yao hazingekuwa tofauti kabisa ikilinganishwa na walivyochukuliwa wahuni waliovamia bunge."