Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ,(TAKUKURU) ,mkoa wa Ilala, imetoa onyo kali kwa waliokuwa wanajimilikisha viwanja na nyumba za urithi kinyume na utaratibu.
Onyo hilo limetolewa leo Januari 15 na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava akiwa anazungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kwa kushirikiana na ndugu wa mbali wa familia kudhulumu viwanja na nyumba zinazoachwa na marehemu nakusema kuwa wameanza kuwasaka na kuwashughulikia watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
“Natoa onyo kwa wale wote ambao wamekuwa wakijimilikisha nyumba na viwanja hasa katika eneo la Kariakoo, tumeanza ufuatiliaji kuwabaini hasa wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu,” amesema Myava.
Aidha Kamanda Myava ametoa onyo kwa waajiri ambao wamekuwa hawapeleki michango ya waajiriwa katika mifuko ya jamii na kusababisha waajiriwa kushindwa kulipwa mafao yao.
“Tayari tumezibaini taasisi mbili na watu binafsi zaidi ya 20 ambao wameshindwa kufanya hivyo na hivyo tunawaomba wengine waweze kuacha tabia hiyo mara moja,” amesema Myava.