Watoto kumi wachanga waliokuwa wametoka tu kuzaliwa wamefariki dunia katika hospitali moja huko nchini India.
Wahudumu wa afya walijitahidi kuwahamishia eneo salama baada ya kutokea kwa moto majira ya asubuhi.
Watoto wachanga saba wameokolewa kabla ya wazima moto kuwasili katika hospitali hiyo ya Bhandara magharibi mwa jimbo la Maharashtra.
Waziri Mkuu Narendra Modi ameelezea tukio hilo kama linalouumiza moyo.
Sababu ya kutokea kwa moto huo bado haijulikani na uchunguzi unaendelea.
Moto huo ulianza takriban saa nane usiku, kulingana na maafisa wa hospitali.
Juhudi za uokozi zilizuiwa na milipuko ambayo ilikuwa inaendelea ndani ya wadi hiyo, kulingana na vyombo vya habari vya eneo.
Muuguzi mmoja aliyekuwa kazini alisema alifahamisha mamlaka kuhusu tukio hilo baada ya kuona moshi unafuka.
"Mamlaka ya hospitali imenusuru watoto saba lakini 10 wamefariki dunia katika ajali hiyo ya kusikitisha," Daktari Pramod Khandate amezungumza na wanahabari.
Katika ujumbe wa Twitter, Bwana Modi ametuma risala zake za rambirambi kwa familia.