Watu sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa katika Kesi ya mauaji ya watu 17




Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa watu sita baada ya kuwakuta na hatia ya mauaji ya watu 17 wa familia yaliyofanyika miaka 10 iliyopita.

Mauaji hayo yalitokea Februari, 2010 ambapo familia ya Kawawa Kinguye na ndugu zake wawili na familia zao walivamiwa usiku na kukatwa mapanga hadi kufa.

Tukio hilo lilitikisa mjini Musoma na kumfanya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru kuangua kilio kwa sauti alipofika eneo la tukio.

Baada ya kuuawa, miili yao ilikutwa na majeraha katikati ya dimbwi la damu huku ng’ombe na kuku nao wakikutwa wamekatwakatwa.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Mustapha Siyani alisema amepitia ushahidi wote wa upande wa utetezi na kukubali kuwa washtakiwa sita kati ya tisa walioshtakiwa walishiriki mauaji hayo bila kuacha shaka.

Kutokana na kujiridhidha huko, Jaji Siyani aliwahukumu kunyongwa hadi kufa na kuwaachia huru wengine watatu baada ya mahakama kuwaona kuwa hawana hatia.

Waliohukumiwa ni Juma Mgaya, Aloyce Nyakumu, Nyakangara Biraso, Marwa Mgaya, Nyakangara Mgaya na Sadok Ikaka huku Magigi Magigi, Kumbata Buruai na Ngoso Ngoso wakiachiwa huru.

Jaji Siyani alisema kutokana ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo imethibitika kuwa watu hao sita walikuwa na dhamira ya kuua akirejea kueleza majeraha waliyokutwa nayo ndugu hao waliouawa.

Alisema adhabu ya mtu aliyeua ni kunyongwa hadi kufa na kwamba, wamehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya adhabu kifungu cha 196,197 sura ya 16.

Washtakiwa hao walifunguliwa mashtaka 17 kila mmoja ambapo, awali watuhumiwa waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo walikuwa ni 19 ambapo, tisa kati yao walifariki dunia wakati kesi hiyo ikiendelea huku mmoja akiachiwa katika hatua za awali.

Kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2018 iliyodumu kwa miaka 10, awali ilifutwa baada ya kukosewa taratibu za ufunguaji wa kesi kisha kufunguliwa upya mwaka 2018.

Katika tukio hilo waliouawa ni Kawawa Kinguye, Bhuki Kinguye, Nyanyama Kinguye, Mericiana Kinguye, Juliana Kinguye, Nyangeta Moris na Umbera Mgaya.

Wengine ni Mgaya Moris, Irene Moris, Nyasimbu Moris, Maheri Moris, Joseph Asophret, Magdalena Moris, Nyarukende Kinguye, Magadalena Kawawa na Dorika Mgaya.

Chanzo cha mauaji

Jaji Siyani alisema chanzo cha mauaji hayo ni kulipiza kisasi baada ya kuuawa watu wawili wakazi wa vijiji vya Buruma na Nyegina wilaya ya Musoma, waliotuhumiwa kuiba mbuzi nyumbani kwa Mgaya mwaka 2005.

Alisema kwa muda mrefu Kawawa Kinguye, ambaye alikuwa mfugaji alikuwa akiibiwa mbuzi mara kwa mara na kwamba, siku moja aliposhuhudia wizi huo alipiga makelele na watu kukusanyika na katika msako waliwakamata watu hao wawili na kuwapiga hadi kufa.

Alibainisha kuwa baada ya mauaji hayo Kawawa alikamatwa na kufikishwa mahakamani na kisha gerezani na wakati akiwa gerezani ndugu wa waliouawa walianza kupanga mikakati ya kulipiza kisasi.

Mwaka 2006 walivamia nyumbani kwa Kawawa na kufanya mauaji ya watu wawili huku Kawawa aliyetoka gerezani mwishoni mwa mwaka 2009 akinusurika.

Alieleza kuwa alipotoka gerezani, mipango ya kummaliza Kawawa na familia yake ilianza kusukwa na mwaka 2010 watu takribani 25 walivamia nyumbani kwa Kawawa na kufanya mauaji ya ndugu hao waliokuwa wakiishi eneo moja.

Mbwa aongoza kubaini mtuhumiwa

Jaji huyo alisema mbwa wa polisi PB Whiteamba 1945 ndiye aliyeongoza operesheni ya kuwasaka wahalifu asubuhi ya siku ya tukio ambapo, alinusa harufu kutoka katika eneo la tukio mtaa wa Mungaranjabo, Manispaa ya Musoma hadi Kijiji cha Nyegina umbali wa kilomita 5.

Jaji Siyani alisema mbwa huyo akiongoza askari watatu alisaidia kufanikiwa kukamatwa kwa Nyakumu na baada ya kufika katika eneo la tukio mbwa huyo alinusishwa jiwe maarufu kama fatuma na kwamba, baada ya kunusishwa alianza kuongoza maaskari katika maeneo tofauti waliyopita wauaji hao.

Alisema mbwa huyo alianzia kwenye nyumba ya Kawawa Kinguye ambako waliuawa jumla ya watu wanane kisha akaelekea kwenye nyumba ya Dorika Mgaya ambapo, waliuawa watu sita kisha aliwaongoza maaskari kuelekea nyumba ya tatu ya Moris Mgaya ambapo, waliuawa watu watatu.

Alisema kuwa baada ya hapo mbwa huyo aliwaongoza askari hadi shambani ambapo, walikuta baadhi ya mali zilizoporwa kwenye tukio hilo zikiwa zimetelekezwa ikiwa ni pamoja na nguo na godoro huku zikiwa na damu.

Alisema mahakama hiyo haikuwa na shaka juu ya utaalamu wa mbwa huyo aliyetambulishwa kama Sajenti Hashimu (sasa marehemu), ambaye naye pia alipata mafunzo ya kuongoza mbwa mafunzo aliyoyapata katika Chuo cha Polisi Moshi mwaka 1988.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad