COASTAL Union ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Yanga, Waziri Junior kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili.
Waziri ameonekana kuwa na wakati mgumu ndani ya kikosi cha Yanga ambapo mpaka sasa ameifungia bao moja pekee, huku kiwango chake kikionekana kuwapa maswali mengi mashabiki na viongozi wa klabu hiyo.
Straika huyo alijiunga na Yanga katika msimu huu akitokea Mbao FC iliyoshuka daraja msimu uliopita ambayo hivi sasa inacheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Coastal iliyo na ushirika na Kampuni ya GSM ambayo inasimamia usajili wa Yanga, ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili huo.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Coastal inamtaka Waziri kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo msimu huu imeonekana kusuasua.“
Coastal huenda ikafanikiwa kuipata saini ya Waziri kwa mkopo wa miezi sita na siyo Ihefu inayotajwa kupeleka maombi ya kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo.
“Kocha wa Yanga Kaze (Cedric) ndiye alipendekeza baadhi watolewe kwa mkopo baada ya kushindwa kuonyesha ushindani wa kupata nafasi ya kucheza, hivyo anaamini wakiondoka huko watapata nafasi ya kucheza na kulinda viwango vyao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema: “Wapo baadhi tuliowatoa kwa mkopo katika dirisha hili dogo, hivyo yeye huenda akawa kati yao lakini kuhusu masuala yote ya usajili tumemuachia kocha.”