Msanii Zuchu aingia kwenye Top 10 ya BBC pamoja na wasanii wengine Afrika wanaopaswa kutazamwa zaidi 2021.
Tumetazama ni nani anayeandaa nini katika mitindo na sauti mbali na ni nani ametoa aina ya muziki ili kutoa orodha ya msanii gani anayepaswa kutazamwa zaidi.
Mwanamuziki huyu huimba kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza na ana sifa za muziki wa Tanzania aina ya Bongo Fleva.
Mwaka uliopita msanii huyu alitoa albamu yake ya uzinduzi I AM Zuchu na pia aliingia kandarasi na Lebo ya kurekodi muziki ya WCB Wasafi.
Kulingna na programu ya kucheza muziki ya Boomplay , Albamu yake ndio iliochezwa sana nchini Tanzania mwaka 2020 na video za muziki wake zimefanikiwa kuvutia mamilioni ya mashabiki katika mtandao wa You Tube.
Fik Fameica (Uganda)
Fik Fameica, ambaye pia anajulikana kama Fresh Boy, ni mmojawapo wa wanamuziki wa muziki wa aina ya Rap waliovutia wengi kutoka Afrika mashariki kwa sasa.
Mara ya kwanza mwanamuziki huyo alipanda katika ulingo wa muziki 2017 akicheza muziki wake Kutama.
Kijana huyo hapigi muziki kama ule unaochezwa na wasanii wengine nchini Uganda na yeye hupiga muziki ambao umeshawishiwa na muziki wa rege.
Fik Fameica anavunja miko na kuungana na vijana wengi kupitia muziki wake na tayari amefanya kolabo na wanamuziki maarufu kutoka kote Afrika akiwemo Patoranking , Vanessa Mdee na Joeboy.
Gaz Mawete (Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo)
Gaz Mawete alianza muziki 2018 kwa kutumia aina ya muziki ya Olingi Nini, na alipanda na kuwa maarufu duniani kwa kupiga muziki wa Kifaransa.
Mchezaji densi huyo wa Dr Congo , ambaye alijipatia umaarufu nyumbani baada ya kushiriki katika mashindano ya kusaka vipaji amepiga kolabo na fally Ipupa ambaye alionekana katika wimbo a C'est Rate.
Mawete pia alishiriki katika albamu ya Dadju Poison au Antidote.
Mawete ameongeza umaarufu wake 2021 baada ya kuteuliwa mwaka uliopita katika orodha ya Best African Act katika tuzo za muziki za MTV barani Ulaya .
Kabza De Small (Africa Kusini)
Kabza De Small amevutia wengi tangu alipoanza kuachilia muziki wake 2016.
Dj huyo na mzalishaji wa muziki amepewa jina la utani la kuwa mfalme wa Amapiano, aina moja ya muziki nchini Afrika kusini.
Muziki wake ni wa kupendeza , wenye nguvu na kuvutia. Kabza De Small amekuwa bingwa wa sauti ambayo inapita katika nchi zingine za Kiafrika na imeanza kukubalika kote ulimwenguni.
Ushawishi wake unaweza kusikika katika nyimbo zilizorekodiwa barani kote na hiyo ilitambuliwa wakati alipochaguliwa katika kitengo cha Best African Act katika tuzo za MTV mwaka uliopita.
KiDi (Ghana)
KiDi, ni sehemu ya kizazi kipya cha wasanii wa Ghana, ambaye alipata mafanikio wakati rekodi yake ya Sugar iliposhinda albamu ya mwaka katika tuzo za muziki za Ghana za 2020.
Muziki wa msanii huyu uliochanganyika na midundo ya Afrika unamfanya kuwa mwanamuziki ambaye muziki wake unaweza kusikilizwa na watu walio nje ya mpaka wa Ghana.
Mnamo mwaka wa 2020, wimbo wa KiDi Say Cheese, kutoka kwa albamu yake Blue , ulimpatia umaarufu wa kimataifa baada ya msanii wa Marekani Teddy Riley kushirikiana naye kwenye remix.
Kijana huyo wa miaka 27 pia ameshirikiana na wasanii wengine wa Afrika Magharibi, pamoja na Davido na Mr. Eazi.
Omah Lay (Nigeria)
Kwa sauti yake ya kupendeza na iliyofafanuliwa vizuri juu ya mchanganyiko wa midundo ya Afrika, Afrofusion na soul, msanii huyo anayekua haraka amejiweka kama mtu wa kutazamwa.
Anaongoza kundi la wasanii wapya wa shule kutoka Nigeria na amefanya kazi na mwimbaji na rapa wa Marekani 6lack.
Mwaka jana Omah Lay alikumbwa na siku chache za matatizo baada ya kuzuiliwa nchini Uganda kwa madai ya kuvunja kanuni za virusi vya corona lakini kampeni kubwa ya mitandao ya kijamii ya kuachiliwa kwake ilikuwa ushahidi na umaarufu wake .
Sha Sha (Zimbabwe)
Sha Sha ni mwimbaji aliyejaliwa na sauti ya Soul, ambayo alijionesha kwenye albamu yake ya Blossom ya 2019.
Sha Sha aliorodheshwa kama mmoja wa wasanii 10 bora wa kike kwenye Spotify huko Afrika Kusini mnamo 2020 wakati kibao chake cha Tender Love kilichomshirikisha DJ Maphorisa na Kabza De Small kiliorodheshwa kama moja ya nyimbo zilizochezwa..
Mwaka jana pia alishinda kitengo cha Best International Act katika Tuzo za BET.
Soraia Ramos (Cape Verde)
Kwa kutumia sauté yake nzuri, Soraia Ramos anaangazia masuala ya mapenzi na uhusiano kupitia lugha ya Kireno na wakati mwingine Creole.
Ameongezea nakshi mtindo wa kizomba na wakati mwingine anaichanganya na mahadhi ya hip-hop na R&B.
Mwimbaji huyo wa Cape Verde kwa sasa anapasua anga na single ya O Nosso Amor aliyotoa kwa ushirikiano na Calema pamoja na remix ya single ya Bai aliyoimba na Lisandro.
Katika mtandao wa YouTube video zake za kibao asili cha Bai na remix zina maoni zaidi ya milioni 15.
Tems (Nigeria)
Anaendela kuwavutia mashabiki wake na kibao cha Try Me alichoachia mwaka 2019, Tems ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo kutoka Nigeria.
Anafahamika kwa sauti yake ya kuvutia, na muziki unaojumuisha miondoko ya soul, hip-hop na R&B.
Kuna uhuru fulani unaomweka juu msanii huyu kutokana na jinsi tungo zake zinavyowasilisha ujumbe unaosisitiza kuwa ni msanii aliyedhibiti himaya yake.
Baada ya kuachia EP yake kwa jina Broken Ears, anaendelea kuvutia mashabiki wake ndani na nje ya Nigeria.
Elaine anachukua kwa kasi nafasi yake kama moja ya sauti za dhahabu za R&B kutoka bara.
Enzi hizi ambazo waimbaji wengi wanatumia teknolojia kuongezea nakshi sauti zao, msanii huyu aliye na umri wa miaka 21- ameamua kutumia sauti yake halisi.
Kusainiwa kwake chini ya lebo ya muziki ya Marekani ya Columbia mwezi Agosti mwaka jana kumemwezesha kujenga msingi imara.
Elaine aliwavutia mashabiki kutokana na uhalisia wake katika kibao chake cha mwaka 2019 kinachofahamika kama 'You're the One'.
Wimbo huu ulimfanya kuwa mmoja wa wasanii wanaotazamwa sana mitandaoni nchini Afrika Kusini.
EP yake ya kwanza ilikuwa kali sana na ilimwasilisha vyema katika ulimwengu wa burudani, kutokana na jinsi ilivyosheheni tungo zilizo na ujumbe wa mapenzi na uhusiano zilizowasilishwa kwa mtindo wa soul na R&B.