22 kutoa ushahidi kesi kina Mdee na wenzake 26






Mashahidi 22 wa upande wa mashtaka, wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi ya kufanya mkusanyiko na kutotii amri halali katika geti la gereza la Segerea, inayowakabili watu 27 wakiwemo wabunge watatu wa viti maalum Chadema.


Ni baada ya upelelezi wa kesi hiyo ya jinai namba 61/2020, kukamilika na washakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH).



Wabunge hao ni Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko ambapo kwa pamoja na wenzao wanakabiliwa na mashtaka saba katika mahakama hiyo.



Mbali na wabunge hao, wengine ni, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, Patrick Assenga na mfanyabiashara, Henry Kilewo.



Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Februari 15, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali.



Akisoma maelezo ya awali Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga na Faraja Ngukah amedai kuwa Machi 13, 2020 maeneo ya gereza la Segerea wilayani Ilala, washitakiwa walifanya mkusanyiko usio halali katika namna ya kuleta hofu na kuvunja amani.



Mkude amedai kuwa katika tarehe hiyo, washtakiwa kwa pamoja hawakutii amri halali iliyotolewa na Ofisa wa Magereza mwenye namba B 3648 Sajent  John aliyewataka wasikusanyike eneo hilo lakini hawakutii na kusababisha kuharibu geti la Magereza, kumjeruhi askari huyo na kumtolea maneno machafu.



Wakili Mkude baada ya kumaliza kuwasomea hoja za awali, hakimu Shahidi aliahiisha kesi hiyo hadi Machi 15, 2021 kwa ajili ya kutajwa na kupanga kusikilizwa kesi hiyo kuanzia Aprili 5 hadi 7, 2021.



Washtakiwa wengine ni Yohana Kaunya mkazi wa Ubungo,  Kedmony Mhembo mkazi wa Salasala, Mshewa Karua mkazi wa Kimara, Khadija Mwago mkazi wa Mtoni Kijichi, Pendo Raphael maarufu kama Mwasomola na mkazi wa Bonyokwa.



Pia yupo, Cesilia Michael mkazi wa Mbezi Mwisho, Happy Abdallah mkazi wa Kawe, Stephen Kitomali mkazi wa Segerea na Paul Makali (40) mkazi wa Majohe.



Kati ya mashtaka saba, yanayowakabili; matatu ni ya kutoa lugha ya kuudhi yanayowakabili, Mdee, Bulaya na Jacob; moja ni kuharibu mali; kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali; kutokutii amri halali iliyowekwa na Jeshi la Magereza na shambulizi.



Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutotii amri halali iliyotolewa na askari Magereza.



Wanadaiwa kutenda kosa hilo, 13 Machi 2020 , eneo la gereza la Segerea lililopo wilaya ya Ilala, kwa makusudi walikaidi amri halali ya kuondoka eneo la gereza kwa amani ili eneo hilo libaki wazi, amri hiyo iliyotolewa na askari mwenye namba B 3648, Sajenti John ambaye ni mlinzi wa geti la gereza hilo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad