Afrika Kusini imesitisha mpangowa kuwachanja watu chanjo ya Oxford-AstraZeneca baada ya utafiti kuonesha matokeo ya "kukatisha tamaa" dhidi ya aina mpya ya Covid ya Afrika Kusini.
Wanasayansi wanasema kuwa maambukizi ya aina hiyo mpya ya corona yamefikia 90% ya visa vipya vya Covid nchini Afrika Kusini .
Utafiti huo, uliowahusisha watu 2000, ulibaini kuwa chanjo hiyo inatoa "ulinzi wa kiwango cha chini sana " dhidi ya wagonjwa wa Covid -19 wanaougua kidogo na wale wanaougua kwa kiwango cha kadri.
Afrika Kusini imepokea dozi milioni moja za chanjo ya AstraZeneca na ilikuwa inatarajia kuanza kuwachanja watu wiki ijayo.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya mtandao Jumapili , Waziri wa afya wa Afrika Kusini Zweli Mkhize alisema kuwa serikali itasubiri ushauri zaidi kuhusu namna itakavyoendelea na chanjo ya Oxford-AstraZeneca baada ya kupata matokeo ya utafiti huo. Majaribio ya chanjo hiyo yalifanyika katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand lakini yalikuwa bado hayajatathminiwa.
Wakati huo huo, alisema kuwa serikali itatoa chanjo zilizotengenezwa na makampuni ya Johnson & Johnson na Pfizer katika wiki zijazo.
"Kwa bahati mbaya, chanjo ya AstraZeneca haifanyi kazi dhidi ya wagonjwa wenye dalili ndogo na za kadri ," alisema Profesa Shabir Madhi, ambaye aliongoza utafiti kuhusu chanjo hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari.
Alisema kwamba utafiti haujaweza kuchunguza ufanisi wa chanjo katika kuzuia maambukizi makali zaidi, kwani washiriki walikuwa na wastani wa umri wa miaka 31, na kwahiyo hawakuwakilisha kundi la watu wanaoweza kuwa na hatari ya kuugua zaidi wanapopatwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Profesa Sarah Gilbert, ambaye aliongoza jopo la uzalishaji wa chanjo ya Oxford, amesema kuwa chanjo hiyo bado inaweza kuwa kinga dhidi ya kuugua sana..
Amesema kuna uwezekano wa watengenezaji wa chanjo hiyo kuifanyia maboresho ili iweze kuwa na ufanisi dhidi ya aina ya corona ya Afrika Kusini ambayo pia inajulikana kama 501.V2 au B.1.351,baadaye mwaka huu.
Wataalamu wanasema kuwa chanjo inaweza kutengenezwa upya na kubadilishwa ili kuiwezesha kukabiliana na aina mpya ya kirusi cha Afrika Kusini kwa kipindi cha wiki kadhaa au miezi kama ni itabidi.
Matokeo ya awali kutoka kampuni ya Moderna yanaonesha kuwa chanjo yake bado ina ufanisi dhidi ya aina mpya ya Covid ya Afrika Kusini E, huku AstraZenica ikisema kuwa chanjo zake zinatoa kinga dhidi ya aina ya corona ya Uingereza ambayo kwa mara ya kwanza ilitambuliwa nchini Uingereza.