Baraza la Madiwani Wilayani Serengeti mkoani Mara limeeleza kusikitishwa na upotevu wa takribani asilimia 80 ya makusanyo ya kodi ya halmashauri huku asilimia 20 pekee ikidaiwa kuingizwa kwenye akaunti ya halmashauri.
Malalamiko hayo yametolewa na baadhi ya madiwani katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wakati wa kikao cha majadiliano na mapendekezo ya makisio ya mpango wa fedha wa bajeti ya mwaka 2021/2022.
Wamesema tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu sasa na kusisitiza iwapo hapatakuwepo na usimamizi madhubuti wa kukusanya mapato na kuziba mianya ya upotevu basi taarifa ya mapitio ya Sh.bilioni 34.3 kama bajeti iliyopitishwa haitoweza kufanikiwa.
Madiwani hao walionyesha wasiwasi wao na kufichua mbinu zinazotumika kukusanya na kufuja mapato pasipo kufikishwa kwenye halmashauri kutokana na utendaji hafifu wa watendaji wanaokusanya mapato.
Akizungumzia suala hilo Diwani wa Kata ya Issenye, Mossi Nyarobi, amesema ni lazima kufanya ukaguzi ili kubaini watumishi wanaokusanya mapato ya halmashauri na kuweka fedha mfukoni bila kufikishwa pahala husika hali inayoikosesha mapato halmashauri na kuwanufaisha watu wachache.
Naye Diwani wa kata ya Kenyamonta alitaka ufanyike ufuatilaji ili kujua sehemu zinazopoteza mapato na kujua kiasi kinachopelekwa halmashauri ili kubaini watendaji waliohusika na hatua za kinidhamu zichukuliwe.
Alisema katika kata yake amebaini fedha zilizopokelewa halmashauri ni tofauti na zilizokusanywa huku kukidaiwa kuondolewa kwa vizuizi njiani vilivyokuwa vinadhibiti utoroshaji wa mazao yanayostahili kulipiwa ushuru.
Alieleza ukusanyaji dhaifu wa mapato ya halmashauri na kuruhusu wafanyabiashara kupita njia za panya umeikosesha mapato wilaya huku baadhi wakidai mashine za kieletroniki kwa ajili kukusanya map ato zinahujumiwa kutotumika kama ilivyokusudiwa.
Naye, Hellena Chacha, ambaye ni Diwani wa Kata ya Ring’wani alisema mianya ya kupotea mapato ipo mingi ikiwemo baadhi ya bidhaa kulipiwa ushuru vma zingine kutolipiwa na kutoa mfano ng’ombe 40 wanaosafirishwa kutoka mnadani ng’ombe 20 wamelipiwa ushuru lakini wengine 20 wanapitishwa bila kulipiwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti Jacob Bega aliwataka madiwani wote kusimamia mapato na matumizi kuhakikisha miradi yite inatekelezwa kwa kiwango.
Katibu wa CCM wilaya ya Serengeti, Peter Mashinji aliwataka watendaji wote kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa kwa ajili maendeleo ya wilaya.