Askofu Kasala: Kifo ni mpango wa Mungu msiwe na wasiwasi
SATURDAY FEBRUARY 06 2021
sababu ya kifo pic
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Fravian Kasala akiongoza ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega
Summary
Sengerema. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Fravian Kasala amesema watu wanatakiwa kutokuwa na wasiwasi kuhusu kifo na kinapotokea watambue kuwa ni mpango wa Mungu.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Februari 6, 2021 katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega iliyofanyika kijiji cha Ngoma Wilayani Sengerema katika kanisa la Mtakatifu Benerdicto.
Amesema kifo cha Kwitega ni mwanzo mpya wa maisha yake mbinguni, “tunapaswa kumwombea na tuyaenzi yote aliyofanya hapa dunia kwa kuwa ameacha alama isiyofutika katika utumishi wake wa umma.”
"Tusali kila siku hatujui siku wala saa ya kuondoka hapa duniani. Maombolezo haya ya leo yasiwe ya kukata tamaa, yalete tumaini jipya kwa mwanadamu. Mwanzo wa kufa ni mwanzo wa maisha mema huko mbinguni, “ amesema Askofu Kasala.
Kwitega alifariki Februari 3, 2021 katika ajali wakati akitoka Arusha kwenda Dodoma baada ya gari alilokuwa amepanda kugongana uso kwa uso na basi. Katika ajali hiyo watu wanne walijeruhiwa ambao ni dereva wake na wanawake watatu waliokuwa kwenye basi hilo.