WIZARA ya mambo ya nje ya Italia imesema kuwa balozi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameuawa katika shambulio dhidi ya msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa Mashariki mwa nchi hiyo.
Balozi Luca Attanasio na mwanajeshi mmoja wa Italia wameuawa katika shambulio lililotokea karibu na mji wa Kanyamahoro. Dereva wa gari, raia wa Congo pia aliuawa katika tukio hilo.
Maafisa katika mbuga ya wanyama ya Virunga wanasema shambulio hilo lilikuwa jaribio la utekaji nyara. Makundi mengi yaliyojihami yanaendesha harakati zake karibu na mbuga hiyo inayopakana na Rwanda na Uganda. Walinzi wa mbuga hiyo wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na kuuawa na waasi.
Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi ametoa taarifa yake ya “rambi ambi kubwa” huku Rais Sergio Mattarella akilaani alichokiita “shambulio la uoga”. Waziri wa mambo ya nje Luigi Di Maio ameelezea “kushtushwa sana na huzuni kubwa ” na mauaji ya “kikatili “
Haijafahamika wazi ni nani aliyekuwa nyuma ya shambulio hilo, lakini makundi mengi yenye silaha yanafahamika kuendesha harakati zake ndani na maeneo yanayozingira mbuga ya wanyama ya Virunga.
Bw Attanasio alikuwa akisafiri kutoka Goma ambako alikwenda kuzuru “mradi wa shule ” katika kijiji cha Rutshuru mashariki mwa nchi hiyo ilisema taarifa ya shirika la WFP lenye makao yake Roma.