MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba amempongeza mwananchi aliyerekodi video, inayoonesha mazingira magumu ya Shule ya Msingi King’ongo.
Kamba alisema hayo jana wakati alipoitembelea shule hiyo iliyopo Kata ya Saranga, Manispaa ya Ubungo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kutembelea miradi mkoani humo kuadhimisha miaka 44 ya CCM.
Chama hicho kilianzishwa Februari 5 mwaka 1977 kwa kuunganisha vyama vya Tanganyika National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP).
Madarasa tisa yamejengwa shuleni hapo, kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilotoa mkoani Kagera baada ya kuona video hiyo mtandaoni.
Katika ujenzi huo, yamejengwa matundu 12 ya choo. Shule hiyo ina wanafunzi 2,500 na ilikuwa na madarasa saba mabovu.
Kamba aliwataka wananchi wa eneo hilo, kutambua kuwa licha ya kauli ya Rais Magufuli kuleta mabadiliko hayo, ni aibu kwao kwa kushindwa kusimamia maendeleo ya shule hiyo.
Alisema, kauli ya serikali kuwa wananchi wasilipe ada haiwazuii kuchangishana kwa maendeleo ya shule wanapokubaliana kupata maendeleo.
“Changamoto za shule hii wananchi mliziona, lakini hamkuona kama ni suala muhimu, mliona ni la kawaida hadi pale alipojitokeza mwananchi aliyerekodi video fupi na kuituma mitandaoni kisha Rais akaona na kutoa maagizo ambayo leo tunayafurahia”alisema Kamba na kuongeza;
“Hii ni aibu yetu wana King’ongo tulitakiwa kuliona suala hili mapema na kulifanyia kazi, hivyo nawataka wananchi sehemu nyingine kushiriki kusaidia kuboresha elimu, serikali inatoa elimu bure kwa maana ya wanafunzi wasilipe ada, lakini haimaanishi kuwa hata yale yetu kama wananchi tusishiriki kuyafanya.”
Aliagiza aliyerekodi video hiyo, asibugudhiwe kwa kuwa ni shujaa wa elimu na alibainisha kuwa CCM Mkoa wa Dar es Salaam itaendelea kuimarisha elimu kwa kuchangia, kuhamasisha na kupigania sekta hiyo kwa hali na mali.
Wanafunzi katika shule hiyo, leo walitajiriwa kuanza kuyatumia madarasa mapya, lakini sasa wanatarajiwa kuingia humo Jumatatu.
Ofisa Habari wa Wilaya ya Ubungo, Joina Nzali, alisema jana ujenzi umekamilika kwa asilimia 99 na kuwa Jumatatu wataanza kuyatumia madarasa hayo yakiwa na madawati.
Madiwani, Wakurugenzi, wabunge, Ma DC/RC...KABLA YA SILINDE MUWE MACHO NA
ReplyDeleteVYANZO VYA MIKUTANO KUTAMBUA ADHA ZA WANANCHI. BADILIKENI KABLA YA MAGU KUKUBADILISHENI. Atakae shindwa kasi yake ni Awe Mtazamaji/Msindikizji NJE