Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango leo Jumanne Februari 23, 2021 amezungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu Rais John Magufuli kusoma ujumbe wa mbunge huyo wa Buhigwe akimueleza kiongozi mkuu huyo wa nchi kuwa anaendelea vyema na matibabu katika hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma.
Akizungumza leo mjini Dodoma, Dk Mpango amemwaga machozi akiwalilia baadhi ya viongozi waliofariki dunia siku chache zilipopita ambao ni aliyekuwa makamu wa kwanza wa rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad; aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi; aliyekuwa mbunge wa Muhambwe, Atashasta Nditiye na Gavana mstaafu wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Dk Mpango amesema amekaa katika hospitali ya Benjamin Mkapa kwa siku 14 baada ya matibabu ya siku 28 huku siku 14 akizitumia katika hospitali hiyo na 14 nyingine akiwa nyumbani kwake.
Amebainisha kuwa kwa sasa afya yake imeimarika baada ya kuondolewa mashine ya kumsaidia kupumua siku tatu zilizopita na ameruhusiwa na madaktari kurejea nyumbani.
Amepongeza huduma nzuri alizopatiwa akisema hakuna haja ya watu kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuwa hospitali za ndani zimeboreshwa.
Februari 19, 2021 katika ibada ya mazishi ya Balozi Kijazi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Magufuli alisoma ujumbe huo wa Dk Mpango akiwataka Watanzania kuacha kutishana.
“Mheshimiwa Rais, asante sana nimepata ujumbe wako kupitia kwa mke wangu, kwa neema ya Mungu naendelea vizuri, ninakula, ninafanya mazoezi ya kifua na kutembea, hao wanaonizushia kifo kwenye mitandao niliwaombea msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.”
“Mheshimiwa Rais Mungu akubariki na akupe neema na ujasiri zaidi katika kuliongoza Taifa letu, katika wimbi hili naungana na wanafamilia katika kuomboleza kifo cha Katibu mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rest in Peace,” amesema Magufuli akimnukuu Dk Mpango.
Mwananchi